• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Raila atafutiwa mfupa

Raila atafutiwa mfupa

NA VALENTINE OBARA

SUALA kuhusu ikiwa kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga, atapewa kiti bungeni limeibuka upya huku vikao vya maridhiano kati ya muungano huo na Kenya Kwanza viking’oa nanga.

Katika vikao hivyo vilivyoanza Jumatano, muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Rais William Ruto, ndio uliowasilisha pendekezo la kuundwa kwa afisi rasmi ya kiongozi wa upinzani pamoja na nafasi ya waziri mkuu.

Vikao hivyo vinasimamiwa na Kiongozi wa Chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, kwa upande wa Azimio na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Taifa, Bw Kimani Ichung’wah, kwa upande wa Kenya Kwanza.

Inatarajiwa kuwa pendekezo hilo likikubaliwa, kiongozi rasmi wa upinzani atakuwa akiwakilisha masuala ya upande wa upinzani akiwa ndani ya bunge naye waziri mkuu pia akipata kiti bungeni kuiwakilisha serikali.

Hata hivyo, uundaji wa afisi rasmi ya kiongozi wa upinzani na ile ya waziri mkuu ndani ya bunge la taifa huenda ukazua kizungumkuti.

Hii ni kutokana na kuwa suala hilo litahitaji urekebishaji wa Katiba kupitia kwa kura ya maamuzi kwani kwa sasa haitambui upande wa serikali wala upinzani bungeni.

Vilevile, likipitishwa kabla ya uchaguzi mkuu ujao, sheria itahitaji kufafanua kama uamuzi huo utatakikana kutekelezwa kuanzia kwa matokeo ya uchaguzi wa 2022 au uchaguzi ujao.

Kimsingi, kiongozi wa upinzani hufaa kuwa aliyeibuka wa pili katika uchaguzi wa urais ambaye kwa muktadha huu ni Bw Odinga.

Kwa upande mwingine, Serikali ya Kenya Kwanza tayari ilimchagua Bw Musalia Mudavadi kuwa kinara wa mawaziri, na kumweka katika nafasi inayoweza kumfanya kuwa waziri mkuu iwapo Katiba itarekebishwa.

Kulingana na Seneta wa Kakamega, Dkt Boni Khalwale, K-Kwanza ilionelea nafasi ya kiongozi rasmi wa upinzani ibuniwe, apewe kiti chake ndani ya Bunge ili mchango wake uwe mkamilifu.

“Kuna upungufu anapoongoza akiwa nje. Akiwa bungeni, atakuwa akienda moja kwa moja hadi katika upande wa upinzani kueleza wazi ajenda zake,” akasema katika mahojiano ya runinga jana Alhamisi.

Mbunge Maalumu wa ODM, Bw John Mbadi, alisema hakuna pingamizi lolote kuhusu pendekezo la kuunda afisi rasmi ya kiongozi wa upinzani.

Bw Mbadi alifafanua kuwa, pendekezo hilo lilikuwa miongoni mwa yale ya Mpango wa Maridhiano (BBI) ambao ulipingwa na viongozi wa Kenya Kwanza.

Hata hivyo, alisema mazungumzo yanayoendelea sasa yangelenga zaidi kutekeleza mambo yanayowezekana bila kuhitaji marekebisho ya Katiba, ndipo yale mengine yanayohitaji Katiba kurekebishwa yaangaliwe baadaye.

Kulingana naye, utekelezaji wa baadhi ya yale ambayo hayahitaji kurekebisha Katiba utawatia moyo wananchi kwamba vikao vinavyoendelea vinazaa matunda.

“Hata katika uchaguzi wa 2027 kutakuwa na mshindi lakini upande ule utakaochukuliwa kama ulioshindwa, utakuwa umepata mamilioni ya kura. Huwezi kuwa na mgombeaji urais aliyezoa mamilioni ya kura kukaa tu huko nje bila nafasi ya kujieleza. Anayeibuka wa pili uchaguzini anafaa kuwa kiongozi rasmi wa upinzani lakini ili kufanya hivyo ni sharti Katiba irekebishwe,” akasema.

Mbali na nafasi ya kiongozi wa upinzani, masuala mengine ambayo Kenya Kwanza inataka yajadiliwe ni kuhusu utekelezaji wa sheria ya usawa wa kijinsia bungeni, marekebisho ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kuwezesha Hazina ya Kustawisha Maeneobunge (CDF) itambuliwe kikatiba, na kuundwa kwa afisi ya Waziri Mkuu.

Mapendekezo sawa na hayo yalikuwa yamewasilishwa na Rais Ruto kwa maspika wa bunge la taifa na seneti mwishoni mwa mwaka 2022.

Muungano wa Azimio ulileta mezani masuala ya kupunguza gharama ya maisha, kuchunguza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2022, kurekebisha IEBC, kuweka sheria za kuzima uvurugaji wa vyama vya kisiasa, na kurekebisha utathmini wa mipaka.

  • Tags

You can share this post!

AMINI USIAMINI: Kuna nyoka mwenye pua kama pembe ya kifaru

Katambe! Ngoma ya EPL yaanza rasmi leo Ijumaa

T L