• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:30 PM
Kenya yanyakua medali kochokocho riadha za barabara duniani

Kenya yanyakua medali kochokocho riadha za barabara duniani

NA GEOFFREY ANENE

PERES Jepchirchir, Sebastian Sawe na Beatrice Chebet walinyakua mataji ya vitengo vyao na kusaidia Kenya kushinda makala ya kwanza ya Riadha za Dunia za Barabarani kwa jumla ya medali nane jijini Riga, Latvia, jana, Jumapilin, Oktoba 1, 2023.

Bingwa wa Olimpiki kilomita 42 Jepchirchir aliongoza Margaret Kipkemboi na Catherine Reline kufagia nafasi tatu za kwanza za 21km, dakika chache kabla ya Sawe, Daniel Simiu na Samuel Mailu kutetemesha umbali huo upande wa wanaume, mtawalia.

Beatrice Chebet na Lilian Kasait walipatia Kenya medali zake za kwanza kwenye mashindano hayo ya zaidi ya mataifa 50 walipokata utepe katika nafasi mbili za kwanza za kilomita tano.

Faith Kipyegon aliridhika na shaba ya maili moja.

Nicholas Kimeli alishindia Kenya medali ya shaba ya 5km. Wakenya walizoa jumla ya tuzo Sh16.5 milioni.

Bingwa wa nusu-marathon duniani mwaka 2016 na 2020 Jepchirchir alipigiwa upatu kutwaa taji na hakusikitisha.

Alifyatuka katika mita 150 za mwisho akimpita Kipkemboi na kushinda kwa saa 1:07:25.

Kipkemboi na Reline walikamilisha kwa 1:07:26 na 1:07:34, mtawalia.

Mshikilizi rekodi ya dunia ya maili moja uwanjani Kipyegon aliridhika na shaba ya maili moja baada ya mbinu zake za kuchomoka mapema kufeli akiduwazwa na Waethiopia Diribe Welteji na Freweyni, mtawalia.

Mkenya Nelly Chepchirchir alikamata nafasi ya nne kwa 4:31.18.

Wakenya hawakuwa na lao katika maili moja ya wanaume baada ya Kyumbe Munguti na Reynold Cheruiyot kumaliza nambari 13 na 22 kwa dakika 4:00.67 na 4:05.91, mtawalia.

Bingwa wa Jumuiya ya Madola mbio za mita 5,000 Chebet alikata utepe kwa dakika 14:35.

Alimpiku Muethiopia Ejgayehu Taye (14:40) aliyekuwa mbele kwa muda mrefu.

Kasait alinyakua fedha kwa 14:39.

Bingwa wa Istanbul Half Marathon, Simiu alichomoka zikisalia kilomita tatu akiridhika na nafasi ya pili kwa dakika 59:14.

Sawe alitawala kitengo hicho kwa 59:10 naye Mailu akafunga tatu-bora (59:19).

Washiriki zaidi ya 340 kutoka mataifa 57 wamekusanyika jijini Riga kwa makala hayo ya kwanza ya siku moja yanayohusisha vitengo vya maili moja, kilomita tano na kilomita 21.

Nambari moja hadi 12 katika vitengo vya nusu-marathon watazawadiwa Sh4.3 milioni, Sh2.1m, Sh1.7m, Sh1.3m, Sh1.1m, Sh1.0m, Sh876,210, Sh730,175, Sh584,140, Sh438,105, Sh292,070 na Sh146,035, mtawalia.

Tuzo ya maili moja na kilomita tano itakuwa Sh1.4m, Sh1.0m, Sh876,210, Sh438,105, Sh365,087, Sh292,070, Sh219,052 na Sh146,035 kutoka nambari moja hadi nane, mtawalia.

Rekodi ya dunia inaandamana na nyongeza ya Sh7.3m.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Kampuni yamlilia Gachagua kuisaidia kurejeshewa ardhi...

Asilimia 70 ya wanaume hutatizika kupata usingizi usiku...

T L