• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 5:50 AM
Kenya yazoa medali 12 ndondi za Afrika Ukanda wa Tatu jijini Kinshasa

Kenya yazoa medali 12 ndondi za Afrika Ukanda wa Tatu jijini Kinshasa

Na GEOFFREY ANENE

KENYA ilikamilisha mashindano ya masumbwi ya Afrika ya ukanda wa tatu na medali 12 (dhahabu moja, fedha tano na shaba sita) jijini Kinshasa katika Jamhuri ya Kidemorkrasia ya Congo mnamo Ijumaa.

Elly Ajowi alishindia Kenya medali yake ya pekee ya dhahabu baada ya kulemea raia wa Cameroon Maxime Yegnong Njieyo katika fainali ya uzani wa zaidi ya kilo 91.

Nahodha wa ‘Hit Squad’ Nick ‘Commander’ Okoth, ambaye hakuwa amepoteza pigano tangu mashindano hayo ya mataifa saba yaanze Machi 22, alisimamishwa na raia wa Cameroon Tchouta Mbianda Ignas Aristide Ron katika fainali ya uzani wa kilo 57.

Christine Ongare alitinga fainali, lakini hakuchapana na Munga Zalia (DR Congo) katika fainali ya uzani wa kilo 51 baada ya daktari kutangaza hayuko fiti kushiriki pigano hilo. Alipata jeraha la jicho katika pigano la awali dhidi ya Zalia.

Boniface Mugunde (uzani wa kilo 69) na David Karanja (uzani wa kilo 52) pia waliridhika na medali za fedha baada ya kupoteza dhidi ya Kayla na Muntu Biakulolowa (wote DR Congo) katika fainali. Joshua Wasike pia aliambulia nishani ya fedha katika uzani wa kilo 91.

Walioshindia Kenya medali za shaba ni Lucy Stacy Ayoma Achieng’ (uzani wa kilo 60), Elizabeth Akinyi (uzani wa kilo 69), Elizabeth Andiego (uzani wa kilo 75), George Cosby Ouma (uzani wa kilo 75), Ediwn Okongo (uzani wa kilo 75) na Hezron Maganga (uzani wa kilo 81).

Timu hiyo chini ya kocha Benjamin Musa iliandaliwa dhifa ya usiku na Balozi wa Kenya nchini DR Congo Dkt George Masafu katika makao yake. Balozi huyo alitunuku Hit Squad zawadi za vitenge kwa bidii waliyoweka katika kupeperusha bendera ya Kenya.

Mataifa yaliyoshiriki mashindano hayo ya kujinoa kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ni DR Congo (wenyeji), Kenya, Msumbiji, Libya, Burundi, Cameroon na Congo Brazzaville.

You can share this post!

Kang’ata sasa akiri ameonja makali ya Covid-19 mara...

Klabu ya Lazio yatozwa faini na rais wake kupigwa marufuku...