• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Kibiwott na Aprot nje ya Riadha za Afrika, Conseslus ndani

Kibiwott na Aprot nje ya Riadha za Afrika, Conseslus ndani

Na AYUMBA AYODI

MSHINDI wa medali ya fedha ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Abraham Kibiwott na malkia wa Afrika mbio za mita 10,000 Alice Aprot wamejiondoa kwenye Riadha za Afrika zitakazofanyika mjini Reduit, Mauritius mnamo Juni 8-12.

Kocha mkuu wa timu ya Kenya Francis “Mfae” Kamau alifichua kuwa wawili hao hawatakuwa katika timu itakayoenda Mauritius mnamo Juni 6 usiku.

Bingwa wa dunia mita 3,000 kuruka viunzi na maji Conseslus Kipruto sasa atapata fursa ya kutetea taji lake la Afrika baada ya kujaza nafasi ya Kibiwott, ambaye ana jeraha la mgongo.

Kipruto, ambaye hakuwa kikosini, amekuwa akifanya mazoezi kwa majuma mawili sasa na alitarajiwa kupima utayari wake katika duru ya riadha za Diamond League ya Rabat, Morocco mnamo Juni 5.

Kipruto alikamata nafasi ya tano wakati wa mashindano ya kitaifa mnamo Aprili 28 na pia kumaliza nafasi hiyo wakati wa mashindano ya kimataifa ya Kip Keino Classic mnamo Mei 7. Kibiwott alishinda mataji hayo.

Bingwa wa Olimpiki 2016 Kipruto sasa atashirikiana na mshindi wa medali ya shaba ya Olimpiki 2020 Benjamin Kigen, ambaye pia ni bingwa wa michezo ya Afrika, na Geoffrey Kirwa.

“Karibu kila mtu alipuzilia mbali Kipruto, lakini amekuwa akifanya vyema sana mazoezini. Nimeridhika naye,” alisema Kamau na kufichua kuwa Aprot ana jeraha la kinena. Purity Komen na Brilliant Chepkorir watabeba matumaini ya Kenya katika mbio za mita 10,000 za kinadada.

Kamau alisema kuwa lengo lao sio tu kuwa nambari moja Afrika nchini Mauritius, bali kuhakikisha watimkaji wa mbio fupi watafuzu kushiriki Riadha za Dunia mnamo Julai 15-24 jimboni Oregon, Amerika na pia michezo ya Jumuiya ya Madola itakayoandaliwa mjini Birmingham, Uingereza mnamo Julai 28 hadi Agosti 8.

Aliongeza kuwa kuwepo kwa mshikilizi wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala na mrushaji mkuki Julius Yego kunapatia timu hiyo motisha.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Kingi afichua siri ya kuungana na Ruto kwa uchaguzi

Jumwa ajipiga kifua baada ya IEBC kumpa cheti

T L