• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Kila akiwa uwanjani, kijana Ryan Ochieng hujitahidi kuiga mbinu za mkali Karim Benzema

Kila akiwa uwanjani, kijana Ryan Ochieng hujitahidi kuiga mbinu za mkali Karim Benzema

NA PATRICK KILAVUKA

CHIPUKIZI Ryan Ochieng,17, ni straika ambaye anashikilia kwamba, Karim Benzema ni kielelezo tena mwenye kila sifa ya kuigwa.

Anaongeza kuwa mchezaji huyo wa Real Madrid humvutia tu kwa mengi.

Kwa mfano; kuchenga kwake, michomo yake kwa makipa na ustadi wa kudhibiti boli akiwa ugani.

Na, kwa vile ujuzi wa fani au taaluma waweza kuigwa, yeye huwa anamtizama katika michuano ya Real Madrid- Ligi ya La Liga ya Uhispania kudondoa mawili matatu ya kuongezea ncha ya kiujuzi.

Aghalabu, apate maarifa ya kuisakatia timu kama Liverpool ambayo yeye ni mfuasi sugu siku za usoni.

Anasema hii ni kutokana na mfumo wa Liverpool ambao unalandana na vile hupenda kunogesha mchezo.

Mwanasoka Ochieng alianza kusakata kabumbu akiwa difenda kabla kuwajibishwa safu ya mashambulizi akiwa timu ya Uthiru Vision chini ya kocha na msimamizi wa timu Philip Odhiambo almaarufu kama ‘Bobo’.

Mwanasoka Ryan Ochieng (wa pili kulia) akiwa na baadhi ya wachezaji wa Uthiru Vision baada ya mechi yao dhidi Sparks FC uwanjani Kihumbuini. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Hata hivyo, alikuwa amechezea timu ya Magic 90 ya Kawangware ya wasiozidi miaka kumi na ile ya waliochini ya 14 akiwa shule ya msingi.

Alisomea Shule ya Msingi ya Ndurarua kabla kujiunga na Shule ya Upili ya Sipala, Bungoma kisha kuguria Sekondari ya Kangemi mwaka huu 2023 Kidato cha Pili.

Akiwa Uthiru Vision ambayo inashiriki Ligi ya Kaunti, Shirikisho la Kandanda Kenya, Nairobi West, ameweza kupanua kipawa chake cha soka kwani amejukumisha kama straika katika kikosi chao cha kwanza na tayari amecheka na nyavu mara nne ligini huku akitoa usaidizi ambao umefanikisha ufungaji wa magoli.

Mwanasoka Ryan Ochieng akipepeta mpira. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Kwa sasa, mfumaji huyo anasema kiu yake  ni kuona anaisaidia timu kuingia tena katika ngarambe ya Ligi ya Kanda, FKF, Nairobi West kwani ni furaha ya kila mchezaji kuona timu inakwea mlima wa kisoka.

Mwanakandanda Ryan anasema wakati wake katika kabumbu ambao ulikuwa wa kujivunia zaidi na wa kumbukumbu kwake, ni wakati walicheza mchuano wa Ligi ya Kaunti, FKF, Nairobi West mwaka huu dhidi ya Huruma Sports na akasawazishia timu yake bao ambalo lilifanya mambo kuwa 1-1 ugani Huruma.

Japo changamoto yake imekuwa kusawazisha masomo na talanta, ameazimia kuchukua fursa hii kuhakikisha anapiga mazoezi vizuri ya kibnafsi na kitimu katika muda wake wa ziada na wakati wa kipindi cha masomo, anazamia masomo kufanikisha malengo yake ya usoni.

Angependa kumkumbuka mchezaji Brian Andenje ambaye amekuwa akimhimiza kucheza boli bila kukata tamaa.

Isitoshe, alimjulisha kwa kocha Odhiambo anayefinyanga talanta yake.

Ujumbe wake ni kwamba, wachezaji ni sharti wajitahidi na kutambua wanachonuia katika bahari pana ya soka.

Isitoshe, wawe wakakamavu kwa sababu hayo ndiyo mambo ambayo yanaweza kuwapatia msukumo wa kusakata boli.

Pia, watatambua mawingu sio mwisho wa kila jambo ila, wajinyanyue kufikia malengo yao.

  • Tags

You can share this post!

Matapeli wa magari kupitia NTSA waona cha mtema kuni

DPP aagizwa awape ushahidi washukiwa wa ulaghai wa dhahabu

T L