• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Kimanzi akiandaa kikosi chake kukabiliana na Tusker

Kimanzi akiandaa kikosi chake kukabiliana na Tusker

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

ALIYEKUWA mkufunzi wa timu ya taifa ya Harambee Stars, Francis Kimanzi amesema anajitayarisha kurekebisha makosa yaliyofanyika kwenye mechi yao na Sofapaka huku akiangazia mechi yao ya Ligi Kuu dhidi ya viongozi wa ligi hiyo, Tusker FC siku ya Ijumaa.

Kimanzi hakuwa na furaha na jinsi wanasoka wake wa Wazito FC walivyocheza kwenye mechi yao ya Ligi Kuu ya BetKing dhidi ya Sofapaka ambapo walifungwa mabao 2-0 kwenye mechi iliyotitigwa katika uwanja wa Dawson Mwanyumba mjini Wundanyi mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kimanzi alisema ingawa hakufurahikia na jinsi walivyocheza, lakini hakutaka kuwalaumu akisema ni kutokana na kukaa kwa siku nyingi bila ya mazoezi ndiko kuliwafanya wanasoka wake kutocheza mchezo wao wa kawaida.

“Siwezi kuwalaumu wachezaji wangu kwa kucheza viwango vya chini kwa kuwa walikaa kipindi kirefu bila ya kufanya mazoezi baada ya kusimamishwa kwa michezo kwa sababu ya kujikinga na uenezaji wa virusi vya corona. Nina imani watarudia hali zao za kawaida karibuni,” akasema.

Mkufunzi huyo anasema Sofapaka walikuwa katika hali nzuri zaidi yao na walistahili kupata ushindi.

“Nina imani kubwa baada ya mechi moja ama mbili zijazo, wanasoka wangu watarudia viwango vya juu sawa na walivyokuwa navyo kabla ya mechi kusimamishwa,” akasema.

Kimanzi anasema kwa wakati huu, anawatayarisha wachezaji wake kwa mechi yao ijayo dhidi ya viongozi wa ligi hiyo, Tusker FC na ana matumaini vijana wake watacheza vizuri zaidi ya walivyocheza na Sofapaka.

“Tunachukulia umuhimu mkubwa kwa kila mechi na tunataka kufanya vizuri kwenye mechi zetu zilizobakia ili tumalize ligi kwenye nafasi nzuri. Tunaamini tutafanya hivyo,” akasema Kimanzi.

Kocha huyo wa Wazito hakutaka kumlaumu Kelvin Kimani kwa kupoteza penalti dakika ya tatu mchezo kuanza ambayo iliokolewa na kipa raia wa Togo, Aigba Moubarak.

“Hata mchezaji awe mzuri namna gani, huweza kupoteza penalti hivyo siwezi kumlaumu Kimani kwa kupoteza penalti yake,” akasema Kimanzi.

You can share this post!

Ahmed Ali Muktar ndiye Gavana mpya wa Wajir

Hatuna ulazima wowote wa kumtimua kocha Pirlo –...