• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Kipchoge azindua wakfu, alenga kuwapa watoto maarifa

Kipchoge azindua wakfu, alenga kuwapa watoto maarifa

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 ya wanaume, Eliud Kipchoge amezindua wakfu wake – Eliud Kipchoge Foundation – mnamo Septemba 9, 2021.

Kupitia mitandao yake ya kijamii, bingwa huyo wa marathon kwenye Olimpiki za 2016 na 2021, amesema kuwa kazi maalum ya wakfu huo ni kuwapa watoto wote duniani uwezo wa kupata maarifa na masomo.

“Nataka watoto wawe katika nafasi itakayofanya siku zijazo wawe watu wazima walio na afya nzuri katika mazingira yaliyo na hewa safi kutoka kwa misitu itakayoweka watu wetu salama. Natumai kuchangia na kuendeleza juhudi za elimu na ulinzi wa mazingira kupitia wakfu wangu. Nataka kufikia watu duniani kupitia sauti yangu,” alisema binadamu huyo wa pekee kuwahi kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya saa mbili.

Malengo yake katika elimu ni: kutoa udhamini wa karo kwa wanafunzi na kuwapa watoto zaidi uwezo wa kupata elimu. Pia, kujenga maktaba na kuwapa watu motisha kwa kuwaonyesha umuhimu wa elimu na nguvu za elimu.

Katika ulindaji wa mazingira, Kipchoge anasema kuwa malengo yake ni kusaidia katika vita dhidi ya misitu kuharibiwa.

Pia, kusaidia katika upanzi wa miti na kutumia shamba kupanda miti na katika uzalishaji wa matunda na mboga.

Isitoshe, kampeni yake pia iko katika kuhifadhi mazingira kwa kizazi kijacho pamoja na kufanya ukimbiaji kuwa maisha ya kila siku kwa watu wengi iwezekanavyo.

Kipchoge, 36, anajivunia rekodi ya dunia ya marathon ya saa 2:01:39 aliyoweka akishinda Berlin Marathon nchini Ujerumani mwaka 2018. Alitimka umbali huo kwa saa 1:59:40 katika mbio maalum za INEOS1:59 Challenge jijini Vienna, Austria mwake 2019.

You can share this post!

Ubelgiji yazamisha Belarus na kufungua mwanya wa alama tisa...

AKILIMALI: Mkenya ajizolea tuzo ya Sh165 milioni atumie...