• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 AM
AKILIMALI: Mkenya ajizolea tuzo ya Sh165 milioni atumie kuimarisha matumizi ya teknolojia miongoni mwa wakulima nchini

AKILIMALI: Mkenya ajizolea tuzo ya Sh165 milioni atumie kuimarisha matumizi ya teknolojia miongoni mwa wakulima nchini

Na WINNIE ONYANDO

MKENYA ni mmoja wa vijana wajasiariamali na wabunifu wa kutumia teknolojia za kisasa katika sekta ya kilimo waliopokea ufadhili wa mamilioni kama njia ya kuimarisha sekta hiyo barani Afrika.

Mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Hello Tractor Bw Jehiel Oliver alitunukwa tuzo ya Sh165 milioni.

Naye mfanyibiashara kutoka Nigeria, Nnaemeka Ikegwuonu ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya ColdHubs alipata ufadhili wa kiasi sawa na cha Mkenya kutoka kwa shirika la Heifer International.

Akizungumza Jumatano katika hafla hiyo jijini Nairobi, Naibu Msimamizi wa Mipango ya Heifer International barani Afrika, Adesuwa Ifedi, alisema kiini cha hatua hiyo ni kuboresha na kupanua sekta ya kilimo miongoni mwa vijana.

“Tukishirikiana na waandalizi wa Shindano la masuala ya Kilimo, Vijana na Teknolojia – Agriculture, Youth and Technology (AYuTe) – tumefurahia jinsi kampuni za ColdHub na Hello Tractor zinavyotumia teknolojia. Kampuni hizo zimejitahidi kuhakikisha wakulima wadogowadogo wa Kiafrika wanapata bidhaa na huduma zinazohitajika kukuza biashara endelevu na zenye faida,” akasema Bi Ifedi.

Tuzo hiyo inakuja siku chache baada ya utafiti uliofanywa ukiwahusisha vijana kuonyesha kuwa asilimia 23 ya vijana kutoka Afrika wanatumia teknolojia ya kisasa katika kilimo.

Bi Ifedi alisema kuna haja ya nchi kuwekeza katika kilimo na kuwahamasisha vijana kuwa wabunifu katika kilimo.

“Baadhi ya wakulima wadogowadogo barani Afrika wanaelewa changamoto zinazowakumba wakulima wasiotumia teknolojia ya kisasa. Hata hivyo, ikiwa watakuwa wabunifu, watabadilisha mapato madogo kutoka kwa kilimo,” akaongeza Bi Ifedi.

Kampuni ya Hello Tractor inawawezesha wakulima walioko vijijini kupata huduma kutoka kwa wmiliki wa trekta kutoka maeneo hayo wanapozihitaji.

Kwa upande mwingine, ColdHub inatoa huduma za kuhifadhi mapato na mavuno katika joto la chini kwenye majokofu ili yasiharibike.

You can share this post!

Kipchoge azindua wakfu, alenga kuwapa watoto maarifa

Vihiga Queens waibuka malkia wa Cecafa, wapokea Sh3m na...