• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Kiptum sasa ndiye mfalme mpya wa marathon duniani

Kiptum sasa ndiye mfalme mpya wa marathon duniani

NA GEOFFREY ANENE

Mkenya Kelvin Kiptum aliendelea kudhihirisha kuwa yeye ni mfalme mpya wa mbio za kilomita 42 baada ya kushinda Chicago Marathon kwa rekodi mpya ya dunia ya saa 2:00:35 nchini Amerika, Jumapili Oktoba 8, 2023.

Kiptum alishikilia nafasi ya pili kwa muda bora katika umbali huo nyuma ya Eliud Kipchoge baada ya kushinda London Marathon nchini Uingereza kwa 2:01:25 mwezi Aprili.

Katika shindano lake la kwanza nchini Amerika na marathon yake ya tatu tu, Kiptum alivunja rekodi ya bingwa mara mbili wa Olimpiki Kipchoge aliyeshinda Berlin Marathon kwa 2:01:09 jijini Berlin nchini Ujerumani mwaka 2022.

Mwezi Mei, Kipchoge, 39, alielezea imani yake kuwa Kiptum, 23, ana uwezo wa kuvunja rekodi ya dunia.

Kiptum alithibitisha hilo baada ya kumtoka Mkenya mwenzake Daniel Mateiko karibu kilomita ya 30 na kufungua mwanya mkubwa kabla ya kukata utepe sekunde 34 ndani ya rekodi Kipchoge alishikilia.

Alifuta pia rekodi ya Chicago Marathon ya wanaume ya 2:03:45 ambayo Mkenya Dennis Kimetto aliweka mwaka 2013.

“Nafurahia sana kupata rekodi ya dunia, ingawa lengo langu lilikuwa kuweka rekodi mpya ya Chicago Marathon. Rekodi ya dunia haikuwa akilini mwangu katika mbio hizi, ingawa niliamini kuwa siku moja nitaimiliki,” alisema.

Kiptum alifuatiwa kwa karibu na bingwa wa Chicago mwaka 2022 Benson Kipruto kutoka Kenya (2:04:02), Mbelgiji Bashir Abdi (2:04:32), Mkenya John Korir (2:05:09) na Muethiopia Seifu Tura (2:05:29).

Nafasi tano za kwanza ziliandamana na tuzo ya Sh14.7 milioni, Sh11.0m, Sh7.3m, Sh4.4m na Sh3.6m, mtawalia.

Kiptum alipata nyongeza ya Sh7.3m kwa kuvunja rekodi ya wanaume ya Chicago.

Mholanzi Sifan Hassan, ambaye pia alishinda London Marathon 2022, alitwaa taji la wanawake kwa rekodi mpya ya Chicago ya 2:13:44 baada ya kufuta ya 2:14:04 ambayo Mkenya Brigid Kosgei aliweka mwaka 2019.

Alimzima Mkenya Ruth Jepchirchir aliyeshinda Chicago mwaka 2021 na 2022.

Jepchirchir aliridhika na nafasi ya pili kwa 2:15:37 nao Muethiopia Megertu Alemu (2:17:09) na Mkenya Joyciline Jepkosgei (2:17:23) wakafunga mduara wa nne-bora.

Makala haya yalivutia washiriki zaidi ya 45, 000.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Kenya yalaza Angola mechi ya kufuzu kombe la dunia wanawake...

Wakazi waambukizwa ugonjwa hatari kwa kutumia maji pamoja...

T L