• Nairobi
  • Last Updated June 1st, 2024 12:49 PM
Kivumbi kushushwa fainali KJ Super Cup

Kivumbi kushushwa fainali KJ Super Cup

Na JOHN KIMWERE

KIVUMBI cha kufa mtu kinatazamiwa kushuhudiwa katika fainali ya kuwania taji la Dagoretti Kusini Super ambalo hudhaminiwa na mbunge wa eneo hilo John Kiarie maarufu KJ.

Wanasoka wa Mainstream Sports Academy kutoka wadi ya Riruta wataingia mzigoni kupepetana na Dagoretti FC kutoka Wadi ya Mutuini ugani Riruta Stadium Kawangware, Nairobi. Nao wanasoka wa Dagoretti Santos watacheza na Home in Home kutafuta mshindi wa nafasi ya tatu.

”Bila shaka tunatarajia mchezo mgumu kwa kuzingatia timu zote zinataka taji la muhula huu,” kocha wa Mainstream, Kadiri Galgalo alisema na kutoa wito kwa kikosi chake kutolaza damu dimbani. Timu hiyo ilitwaa tiketi ya kushiriki mchezo huo baada ya kucharaza Home in Home kutoka wadi ya Waithaka kwa mabao 3-0 kwenye nusu fainali.

Wafungaji wa Mainstream walikuwa Robin Aseneka aliyecheka na wavu mara mbili huku Regan Onyanzi akifuma bao moja. Kwenye nusu fainali ya pili Dagoretti Youth iliangusha Dagoretti Santos kwa goli 1-0 lililofungwa na Johnstone Macharia.

Mashindano hayo ya makala ya tatu yalishirikisha timu 72 kutoka wadi zote tano katika eneo mbunge la Dagoretti Kusini. Mshindi wa ngarambe hiyo atapokea Sh100,000, nafasi ya pili itatuzwa Sh50,000 huku nafasi ya tatu ikipongezwa kwa Sh25,000.

You can share this post!

Shari Afrika awaza kubeba tuzo ya Grammys

Koth Biro: Patashika sita kupigwa wikendi hii

T L