• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Klopp na Pep watofautiana kuhusu pendekezo la Kombe la Dunia kuandaliwa kila baada ya miaka miwili

Klopp na Pep watofautiana kuhusu pendekezo la Kombe la Dunia kuandaliwa kila baada ya miaka miwili

Na MASHIRIKA

KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool na Pep Guardiola wa Manchester City wametofautiana kuhusu mipango ya kuandaliwa kwa fainali za Kombe la Dunia kila baada ya miaka miwili.

Huku Klopp akikosoa pendekezo hilo kwa kusisitiza kwamba “ni suala linalosukumwa kwa sababu ya tamaa ya pesa”, Guardiola amelichangamkia na kuunga mkono.

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa sasa linakusanya maoni ya wadau kuhusu mpango wa kufutiliwa mbali kwa utaratibu wa kuandaliwa kwa fainali za Kombe la Dunia kwa wanaume na wanawake kila baada ya miaka minne.

Tayari klabu, ligi na vinara wengi wa mashirikisho mbalimbali ya soka wamepinga pendekezo hilo japo kuna wadau, akiwemo Guardiola, wanaounga mkono mpango huo wa FIFA.

“Huwezi kuharamisha wazo. Mashindano ya Kombe la Dunia hayana mfano. Kama shabiki wa soka, napenda sana kutazama mechi, hivyo itapendeza sana iwapo uhondo huo utakuwa ukija kila baada ya miaka miwili,” akasema Guardiola ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Barcelona na Bayern Munich.

Arsene Wenger ambaye ni mkufunzi wa zamani wa Arsenal ndiye anayesukuma zaidi mpango wa kubadilishwa kwa utaratibu wa sasa wa kuandaliwa kwa fainali za Kombe la Dunia. Mkufunzi huyo raia wa Ufaransa kwa sasa ndiye kinara wa FIFA anayesimamia maendeleo ya soka duniani.

Kwa mujibu wa Wenger, kutekelezwa kwa pendekezo hilo jipya kutashuhudia idadi kubwa ya likizo fupi zinazochukuliwa na ligi mbalimbali kupisha mechi za kimataifa ikipungua japo safari za mara kwa mara za wachezaji zitaongezeka.

“Kalenda ya sasa imepitwa na wakati. Utaratibu uliopo uliasisiwa 1930 japo kuna mataifa 133 ambayo hayajawahi kunogesha fainali za Kombe la Dunia,” akatanguliza Wenger.

“Soka si mchezo tu kwa ajili ya burudani. Pia ni kitega-uchumi na ni vyema tuzindue mbinu za kuimarisha mchezo huo na kutoa majukwaa mengi iwezekanavyo yatakayochangia ustawi na makuzi ya kandanda kimataifa,” akaongeza.

“Sote tunajua lengo la pendekezo hili. Kiini chake ni tamaa ya pesa. Hata hivyo, utasikia baadhi ya watu ‘wakitetea uongo’ kwamba madhumuni ni kutoa fursa kwa mataifa mengi kujiweka pazuri kushiriki Kombe la Dunia. Hawa ni watu wasiojali kabisa maslahi ya wachezaji,” akasema Klopp.

Mtazamo wa Klopp unaungwa mkono na kocha wa sasa wa Crystal Palace, Patrick Vieira aliyewahi kuchezea Arsenal pamoja na kuongoza Ufaransa kunyanyua Kombe la Dunia mnamo 1998.

Zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wa Uingereza, wengine wanaopiga pendekezo hilo la FIFA ni kinara wa La Liga Javier Tebas, rais wa Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) Aleksander Ceferin na wasimamizi wa Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (CONMEBOL).

Kwa mujibu wa rais wa FIFA, Gianni Infantino, pendekezo la kubadilishwa kwa utaratibu wa sasa wa kuandaa fainali za Kombe la Dunia limeungwa mkono na mashirikisho 166 ya soka kutoka mataifa mbalimbali duniani na kupingwa na mashirikisho 22 pekee.

Fainali za Kombe la Dunia kwa upande wa wanaume zimekuwa zikiandaliwa kila baada ya miaka minne tangu 1930 isipokuwa mwaka wa 1942 na 1946 kwa sababu ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Fainali hizo kwa upande wa wanawake zimekuwa zikiandaliwa kila baada ya miaka minne tangu 1991.

Kubadilishwa kwa jinsi ambavyo kipute hicho kitakuwa kikiendeshwa hadi kuwa kila baada ya miaka miwili kutaathiri michuano mingine ya kimataifa kama vile Euro ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne, miaka miwili kabla na baada ya fainali za Kombe la Dunia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Matiang’i chini ya ulinzi mkali

GUMZO LA SPOTI: Real Madrid yapanga usajili wa nguvu kwenye...