• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 6:50 AM
Kocha Jurgen Klopp asema ataondoka Liverpool mnamo 2024

Kocha Jurgen Klopp asema ataondoka Liverpool mnamo 2024

Na MASHIRIKA

KOCHA Jurgen Klopp amefichua mpango wa kuondoka Liverpool mnamo 2024 mkataba wake wa sasa na miamba hao wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) utakapotamatika rasmi.

Mkufunzi huyo raia wa Ujerumani alipokezwa mikoba ya Liverpool mnamo 2015 baada ya kuondoka kwa Brendan Rodgers aliyeyoyomea Celtic ya Scotland kabla ya kurejea Uingereza kuwatia makali vijana wa Leicester City.

Tangu atue ugani Anfield, Klopp aliongoza Liverpool kutwaa taji la sita la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2019 baada ya kukomoa Tottenham Hotspur katika fainali iliyofanyika jijini Madrid, Uhispania.

Katika msimu uliofuata wa 2019-20, Klopp aliongoza waajiri wake kunyanyua taji la EPL kwa mara ya kwanza baada ya ukame wa miaka 30.

Ameongoza Liverpool pia kutia kapuni mataji ya Uefa Super Cup na Kombe la Dunia. Taji la hivi karibuni zaidi ambalo alishindia kikosi chake ni Carabao Cup baada ya kupepeta Chelsea kwa penalti 11-10 ugani Wembley mnamo Februari 27, 2022.

“Mpango wangu ni kuondoka Anfield mnamo 2024 na kurejea Ujerumani kufanya mambo mengine. Hivyo ndivyo tumeagana na waajiri wangu. Sioni tatizo lolote hapo,” akasema Klopp ambaye pia amekuwa akihusishwa pakubwa na uwezekano wa kuyoyomea Uhispania kudhibiti mikoba ya Real Madrid.

Klopp amewahi pia kudhibiti mikoba ya Eintracht Frankfurt (1987-1988), Mainz (2001-2008) na Borussia Dortmund (2008-2015).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Manaibu wajitafutia pa kujisitiri uchaguzini

WANDERI KAMAU: Mzozo Ukraine umeibua upya Vita Baridi...

T L