• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 6:50 AM
Kocha Mulee asema Gaspo Women wameweka macho kwa Kombe la FKF

Kocha Mulee asema Gaspo Women wameweka macho kwa Kombe la FKF

NA AREGE RUTH

KOCHA mkuu wa Gaspo Women Jacob ‘Ghost’ Mulee anasema timu yake ina uwezo wa kutinga raundi ya nane ya kombe la Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) wikendi hii.

Gaspo watakabana koo na Nakuru City Queens katika raundi ya 16 ambayo imepangwa kuchezwa Aprili 15, 2023 katika uwanja wa Maonyesho ya Kilimo (ASK) Kaunti ya Nakuru.

Gaspo walivuna ushindi mnono wa 3-0 dhii ya Zetech Sparks wikendi iliyopita katika mechi ya ligi iliyosakatwa ugani GEMS Cambridge.

Mulee ambaye alijiunga na timu hiyo wiki mbili zilizopita alidai kuwa, ushindi huo uliwapa morale kuendelea kujifua mazoezini wiki hii.

“Tunafuraha kwamba tumepata pointi tatu na furaha zaidi kwamba hatukuruhusu kufungwa bao. Hii imeleta morali kwa timu na tunarudi kujiandaa kwa kombe la FKF,” Mulee alisema.

“Mechi za mwondoano ni ngumu kwa sababu hakuna mnyonge. Tutakuwa ugenini kucheza na Nakuru, hii ni timu ngumu. Hatutawadharau kwa sababu lolote linaweza kutokea, tutajaribu kutumia nafasi zetu vizuri,” aliongeza Mulee.

Robo fainali imepangwa kufanyika Mei 20, 2023. Mechi za nusu fainali zitafanyika Juni 24, 2023, na fainali itachezwa Julai 2, 2023.

Zikiwa zimesalia mechi nane msimu wa 2022/23 Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) kukamilika, Gaspo wanaongoza kileleni mwa jedwali na alama 34.

Mabingwa mara tatu KWPL Vihiga Queens wanafuata nafasi ya pili na alama sawa lakini wanatafutiana na mabao.

  • Tags

You can share this post!

Kenya kuandaa Cecafa ya wasiozidi umri wa miaka18

Dalai akemewa kwa kutaka mtoto amnyonye ulimi

T L