• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Kocha wa Bayern asema anatishiwa maisha baada ya kikosi chake kuaga UEFA

Kocha wa Bayern asema anatishiwa maisha baada ya kikosi chake kuaga UEFA

Na MASHIRIKA

KOCHA Julian Nagelsmann amesema ametishiwa maisha kupitia mitandao ya kijamii baada ya waajiri wake Bayern Munich kudenguliwa na Villarreal ya Uhispania kwa jumla ya mabao 2-1 kwenye robo-fainali za soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Bayern ambao ni miamba wa soka kutoka Ujerumani, walipokezwa na Villarreal kichapo cha 1-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa robo-fainali za UEFA nchini Uhispania kabla ya kuambulia sare ya 1-1 kwenye marudiano ugani Allianz Arena.

“Nilitarajia kushambuliwa na wakosoaji. Hilo ni jambo la kawaida kila mara kikosi cha haiba kubwa kinapodenguliwa na ‘wanyonge’ kiputeni,” akatanguliza Nagelsmann, 34.

“Lakini ukawaida hupotea kabisa na nafasi yake kutwaliwa na hofu zaidi iwapo utapokea jumbe 450 za kukutishia maisha kupitia Instagram. Si rahisi kupitia hali kama hiyo,” akaongeza kocha huyo wa zamani wa RB Leipzig.

Huu ni msimu wa kwanza kwa Nagelsmann kudhibiti mikoba ya Bayern tangu aaminiwe kuwa mrithi wa mkufunzi Hansi Flick aliyebanduka msimu uliopita wa 2020-21 na kuanza kutia makali timu ya taifa ya Ujerumani.

Bayern wanapigiwa upatu wa kuhifadhi taji la Bundesliga na kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 69, tisa zaidi kuliko nambari mbili Borussia Dortmund.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Southampton yaendeleza masaibu ya Arsenal

Hatimaye Shahbal akubali kuunga Nassir ugavana

T L