• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Mteremko kwa Ubelgiji na Brazil, Uhispania na Ujerumani wakitarajiwa kuhema katika hatua ya makundi

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Mteremko kwa Ubelgiji na Brazil, Uhispania na Ujerumani wakitarajiwa kuhema katika hatua ya makundi

Na MASHIRIKA

JAPO Uhispania na Ujerumani wanatarajiwa kusonga mbele kwa wepesi kutoka Kundi E katika Kombe la Dunia nchini Qatar, wana ulazima wa kujituma maradufu ili kuzima ndoto za Japan na Costa Rica.

Japan walitinga raundi ya 16-bora ya Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi ila wakadenguliwa na Ubelgiji. Costa Rica kwa upande wao waliduwaza Uingereza, Italia na Uruguay katika Kundi D kwenye Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil kabla ya kubandua Ugiriki katika raundi ya 16-bora.

Ujerumani watafungua kampeni zao za Kundi F dhidi ya Japan mnamo Novemba 23 ugani Khalifa, siku moja kabla ya Uhispania kumenyana na Costa Rica uwanjani Al Thumama.

Fainali za Qatar ni za 21 kwa Ujerumani kunogesha. Kikosi hicho kinachonolewa na mkufunzi Hansi Flick kimenyanyua Kombe la Dunia mara nne (1954, 1974, 1990, 2014) na sasa kinashikilia nafasi ya 11 kimataifa.

Uhispania (nambari saba) watakuwa wakiwania taji hilo kwa mara ya pili katika jaribio la 17 baada ya kutwaa ubingwa mnamo 2010 nchini Afrika Kusini. Costa Rica (31) wameshiriki Kombe la Dunia mara tano huku nambari 24 Japan wakijivunia kunogesha kivumbi hicho mara saba.

Chini ya kocha Roberto Martinez, Ubelgiji wanatazamiwa kuteremkia Croatia, Morocco na Canada kirahisi. Kikosi hicho ambacho ni cha pili kimataifa, kinajivunia huduma za wanasoka wakiwemo Thibaut Courtois, Kevin de Bruyne, Eden Hazard na Romelu Lukaku.

Morocco (22) wataanza kampeni dhidi ya Croatia (12) mnamo Novemba 23 ugani Al Bayt, saa chache kabla ya Ubelgiji wanaowinda Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza kushuka uwanjani Ahmad bin Ali kuvaana na Canada (41). Hii ni mara ya 15 kwa Ubelgiji kushiriki Kombe la Dunia, mara ya saba kwa Croatia na ya saba kwa Morocco.

Kundi G linajumuisha Uswisi (15), Cameroon (43), Serbia (21) na Brazil wanaoshikilia nafasi ya kwanza kimataifa. Brazil watafungua kampeni dhidi ya Serbia ugani Lusail Iconic mnamo Novemba 24, saa chache kabla ya Uswisi kukwaryzana na Cameroon.

Brazil waliotwaa Kombe la Dunia mara tano (1958, 1962, 1970, 1994, 2002) wameshiriki kipute hicho mara 22 na watategemea zaidi maarifa ya Neymar Jr, Thiago Silva na Alisson Becker. Ni mara ya nane kwa Cameroon kunogesha kipute hicho na mara ya 13 kwa Serbia na Uswisi.

MAKUNDI YA KOMBE LA DUNIA:

KUNDI E: Uhispania, Costa Rica, Ujerumani, Japan

KUNDI F: Ubelgiji, Canada, Morocco, Croatia

KUNDI G: Brazil, Serbia, Uswisi, Cameroon

KUNDI H: Ureno, Ghana, Uruguay, Korea Kusini

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali ieleze iwapo kuna ongezeko la maambukizi...

Aliyefungua zipu ya jaketi ya polisi mwanamke ashtakiwa

T L