• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:55 PM
KOMBE LA DUNIA: Raphinha abeba Brazil dhidi ya Uruguay

KOMBE LA DUNIA: Raphinha abeba Brazil dhidi ya Uruguay

Na MASHIRIKA

BRAZIL ambao ni mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia walikaribia kufuzu kwa makala yajayo ya kipute hicho baada ya kukung’uta Uruguay 4-1 mnamo Oktoba 15, 2021 katika uwanja wa Amazonia mjini Manaus.

Mchuano huo ulimpa fowadi wa Leeds United, Raphinha Belloli, 24, fursa ya kufungia Brazil mabao yake ya kwanza kimataifa huku mengine yakijazwa kimiani kupitia Neymar na Gabriel Barbosa Almeida baada ya Luis Suarez kufungia Uruguay.

Kufikia sasa, Brazil wanaongoza orodha ya vikosi 10 vya Amerika Kusini kwa alama 31, sita zaidi kuliko nambari mbili Argentina waliotandika Peru 1-0 kupitia juhudi za mshambuliaji matata wa Inter Milan, Lautaro Martinez.

“Nimetimiza ndoto zangu za tangu utotoni. Ni tija na fahari tele kufungia Brazil mabao mawili katika gozi hili muhimu,” akasema Raphinha aliyekuwa akianza mechi ya Brazil kwa mara ya kwanza.

Kwingineko, Brereton Diaz wa Blackburn Rovers alipachika wavuni mabao mawili na kusaidia Chile kunyuka Venezuela 3-0. Diaz kwa sasa amefungia Chile magoli matatu kutokana na mechi nane zilizopita tangu awajibishwe kwa mara ya kwanza katika mchuano wa kimataifa mnamo Mei mwaka huu.

Ushindi dhidi ya Venezuela ulipaisha Chile hadi nafasi ya sita jedwalini kwa alama 13, moja kuliko Bolivia waliotandika Paraguay 4-0. Paraguay pia wamejivunia alama 12 kutokana na mechi 12 zilizopita japo pengo la pointi tano linatamalaki kati yao na nambari tatu Ecuador. Colombia na Uruguay wanashikilia nafasi za nne na tano mtawalia kwa alama 16 kila mmoja.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

PSG waendeleza ubabe wao bila Neymar na Messi

Walioathirika kutokana na kero ya nzige wanaendelea kupata...

T L