• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Korir avunia Kenya fedha marathon ya dunia nchini USA

Korir avunia Kenya fedha marathon ya dunia nchini USA

NA GEOFFREY ANENE

KENYA iliridhika na medali ya fedha katika marathon za kinadada kupitia kwa Judith Jeptum Korir kwenye Riadha za Dunia mjini Eugene, Oregon, Jumatatu.

Katika mbio hizo za kilomita 42 nchini Amerika (USA), bingwa mtetezi Ruth Chepng’etich alijiuzulu kabla ya kufika katikati baada ya kuumwa na tumbo.

Korir akatwaa uongozi na kuwa beba kwa bega na Gotytom Gebreslase kwa zaidi ya kilomita 10, kabla ya Muethiopia huyo kumtoka chini ya kilomita mbili za mwisho na kutwaa taji kwa saa 2:18:11.

Bingwa wa Paris Marathon, Korir, aliridhika na fedha kwa saa 2:18:20 ambao ni muda wake bora.

Naye Mwisraeili mzawa wa Kenya, Lonah Chemtai Salpeter, akakamilisha tatu-bora (2:20:18).

Angela Tanui, ambaye sawa na Chepng’etich walikuwa katika orodha ya waliopigiwa upatu kutwaa medali, alimaliza nafasi ya sita (2:22:16).

Tukienda mitamboni, Kenya ilikuwa na medali tatu za fedha na shaba moja.

Stanley Mburu alipatia Kenya medali ya tatu usiku wa kuamkia jana alipoandikisha muda wake bora msimu huu kwa kunyakua fedha mbio za mita 10,000 akitumia dakika 27:27.90.

Nyota Hellen Obiri na Marget Chelimo pia walizoa fedha na shaba katika mbio hizo za kuzunguka uwanja mara 25, katika kitengo cha kinadada siku ya pili ya mashindano Jumamosi.

Mburu alimaliza nyuma ya Joshua Cheptegei (27:27.43) na mbele ya Mganda mwingine Jacob Kiplimo (27:27.97).

Mkazi huyo wa Japan alifanya kazi ya ziada katika 100m za mwisho kumbandua Muethiopia Selemon Barega kutoka hesabu ya medali ya fedha.

Bingwa mtetezi wa 1,500m Timothy Cheruiyot na Abel Kipsang watakimbia fainali yao hapo kesho.

Mapema leo itakuwa zamu ya Conseslus Kipruto kutetea taji lake la dunia kwenye fainali ya 3,000m kuruka maji na viunzi; atashirikiana na Abraham Kibiwot na Leonard Bett.

Malkia wa 1,500m Faith Kipyegon na Winny Chebet pia watajibwaga uwanjani mapema leo kwa fainali ya fani yao.

Mkenya Moitalel Mpoke aliaga mbio za 400m kuruka viunzi katika awamu ya nusu-fainali hapo jana.

You can share this post!

KWA KIFUPI: Chumvi nyingi kwenye chakula hatari kwa afya...

Red Devils wamnyaka Martinez wa Ajax

T L