• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Leeds United wamfuta kazi kocha Gracia na kuajiri mkongwe Sam Allardyce

Leeds United wamfuta kazi kocha Gracia na kuajiri mkongwe Sam Allardyce

Na MASHIRIKA

LEEDS United wamemfuta kazi kocha Javi Gracia na kumpokeza mikoba mkufunzi wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, Sam Allardyce katika juhudi za kukwepa kushuka daraja kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2022-23.

Gracia ambaye ni raia wa Uhispania, aliteuliwa kudhibiti mikoba ya Leeds mnamo Februari 2023 na ametimuliwa baada ya wiki 10 pekee. Hadi kufurushwa kwake, alikuwa amesimamia mechi 12 uwanjani Elland Road.

Allardyce, 68, sasa ana kibarua kizito cha kuongoza Leeds wanaoshikilia nafasi ya 17 jedwalini kujiondoa kwenye mduara wa vikosi vinne vya mwisho. Leeds wamesakata jumla ya mechi 34 na wanajivunia alama 30 sawa na Leicester City na Nottingham Forest. Everton wanakamata nafasi ya 19 kwa pointi 29, tano kuliko Southampton wanaovuta mkia baada ya kutandaza pia michuano 34.

Kibarua cha kwanza cha mkufunzi Allardyce kambini mwa Leeds ni mchuano dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City mnamo Jumamosi ya Mei 6, 2023 uwanjani Etihad.

Allardyce ambaye msaidizi wake atakuwa kocha wa zamani wa MK Dons, Charlton na Oxford United, Karl Robinson, alisema ilimchukua sekunde chache sana kukubali kazi ya kuwa kocha wa Leeds.

“Nilishangaa sana. Sikuwa kufikiria kwamba katika hatua hii ya msimu hili suala la mimi kuwaziwa kurejea katika ulingo wa ukufunzi lingefanyika. Nilidhani hakungekuwa na kazi,” akatanguliza.

“Ningefikiria zaidi kuhusu fursa hiyo ya Leeds. Lakini ilikuja wakati ambapo hilo lisingewezekana. Tuna mechi nne ambazo tunataka kucheza kama fainali ili kikosi kisalie katika EPL,” akasema.

Gracia aliteuliwa kuwa mkufunzi wa Leeds mnamo Februari 21, wiki mbili baada ya kutimuliwa kwa kocha wa zamani wa kikosi hicho, Jesse Marsch, aliyepigwa kalamu chini ya mwaka mmoja baada ya kujaza pengo la Marcelo Bielsa.

Mechi ya mwisho kwa Gracia, 52, kusimamia kambini mwa Leeds ilikuwa dhidi ya Bournmourh waliowapepeta 4-1 mnamo Aprili 30, 2023.

Mechi hiyo ilikuwa ya hivi karibuni zaidi kushuhudia Leeds wakipokezwa kichapo kinono chini ya kocha huyo wa zamani wa Watford. Leeds waliwahi pia kupepetwa 6-1, 5-1 na 4-1 na Liverpool, Crystal Palace na Arsenal mtawalia mnamo Aprili 2023.

Kikosi hicho sasa hakijashinda mechi yoyote kai ya tano mfululizo zilizopita huku wakipoteza michuano minne tangu wasajili ushindi wa 2-1 dhidi ya Nottingham Forest mnamo April 4, 2023.

Gracia aliyeongoza Watford kutinga fainali ya Kombe la FA mnamo 2019, aliwahi pia kudhibiti mikoba ya Valencia (Uhispania) na Al Sadd (Qatar). Alishinda mechi tatu kati ya 12 alizosimamia kambini mwa Leeds.

Kwa upande wake, Allardyce hajakuwa akinoa kikosi chochote tangu msimu wa 2020-21 wakati ambapo waliokuwa waajiri wake West Bromwich Albion waliteremshwa ngazi kwenye EPL. Hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kushuka daraja ligini katika taaluma ya ukocha.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

  • Tags

You can share this post!

Washambulizi Harambee Starlets wang’aa TZ na Rwanda

Naibu chifu atiwa mbaroni akidaiwa kunajisi bintiye chifu

T L