• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Washambulizi Harambee Starlets wang’aa TZ na Rwanda

Washambulizi Harambee Starlets wang’aa TZ na Rwanda

NA AREGE TUTH

MSHAMBULIZI mahiri wa Harambee Starlets Jentrix Shikangwa, ndiye Mchezaji Bora wa mwezi Machi Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Lite (SLWPL) nchini Tanzania.

Kufikia sasa, Mkenya huyo ndiye Mfungaji Bora wa ligi hiyo akiwa na mabao 13 kutokana na mechi 15 akiwa na klabu ya Simba Queens.

Shikangwa amekuwa katika fomu nzuri tangu alipoachana na timu ya Fatih Karagumruk ya Uturuki mwaka 2022.

Naye mshambulizi mwingine wa Starlets, Judith Atieno Jumanne, alifungia timu yake ya Rayon Sports mabao matano, walipoigaragaza ES Mutunda 10-0 katika nusu fainali ya mkondo wa kwanza wa Kombe la Amani la Rwanda kwa Wanawake katika uwanja wa Skolx jijini Kigali.

Licha ya kujiunga na timu hiyo katika kipindi cha pili cha msimu, kwa sasa anakuwa mfungaji bora wa pili wa klabu hiyo akiwa amefunga mabao 42 na kupeana asisti 19 katika michezo 19.

Wikendi iliyopita, Rayon ilipandishwa daraja hadi Ligi Kuu ya Wanawake ya Rwanda Divisheni ya Kwanza baada ya kuchapa Nasho FC 10-1.

Atieno alifunga mabao mawili na kutoa usaidizi mara mbili.

“Nina furaha kwamba tulipandishwa daraja la juu. Kucheza katika Ligi Daraja la Pili haikuwa rahisi, lakini tulijitolea kwa uwezo wetu wote. Ninasubiria kucheza katika daraja la juu msimu ujao na kufunga mabao zaidi,” aliongeza.

Akizungumza na Taifa Spoti, Katibu Mkuu wa Rayon Sports, Patrick Namenye alisema anafurahi kwamba imeichukua timu hiyo msimu mmoja tu kupanda daraja la kwanza.

“Kila mmoja katika klabu anajivunia wachezaji wetu na kufurahishwa na mafanikio hayo,” alisema Namenye.

Atieno pia yuko kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi Machi pamoja na washambuliaji Mukeshimana Dorothee na Imanizabayo Florence.

“Kuanzia Machi tutakuwa tukitoa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi kwa timu yetu ya wanawake. Mshindi atapata vifaa vya mazoezi na hundi ya takriban Sh13,000,” aliongeza Namenye.

  • Tags

You can share this post!

Barcelona sasa pua na mdomo kutawazwa mabingwa wa La Liga...

Leeds United wamfuta kazi kocha Gracia na kuajiri mkongwe...

T L