• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 1:20 PM
Leeds United yadidimiza matumaini ya Spurs kushiriki soka ya bara Ulaya msimu ujao

Leeds United yadidimiza matumaini ya Spurs kushiriki soka ya bara Ulaya msimu ujao

Na MASHIRIKA

PATRICK Bamford alifungia Leeds United bao muhimu dhidi ya Tottenham Hotspur mbele ya kocha wa timu ya taifa ya Uingereza, Gareth Southgate na kusaidia waajiri wake kusajili ushindi wa 3-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi.

Matokeo hayo uwanjani Elland Road, yalididimiza zaidi matumaini ya Spurs kushiriki soka ya bara Ulaya msimu ujao wa 2021-22.

Stuart Dallas aliwaweka Leeds kifua mbele kwa kufunga goli lake la nane msimu huu katika dakika ya 13. Kiungo huyo raia wa Northern Ireland, alichuma nafuu kutokana na mpira uliopanguliwa na kipa Hugo Lloris wakati akijaribu kumzuia beki Sergio Reguilon kujifunga.

Hata hivyo, uongozi huo wa Leeds ulidumu kwa dakika 12 pekee kwa kuwa fowadi raia wa Korea Kusini, Son Heung-min alisawazisha mambo baada ya kushirikiana vilivyo na kiungo Dele Alli.

Hata hivyo, Leeds walirejea kifua mbele kupitia goli la Bamford aliyejaza kimiani krosi ya Ezgjan Alioski kabla ya Rodrigo kutokea benchi na kuhakikisha kwamba Spurs wanapokezwa kichapo cha kwanza ligini baada ya mechi tatu chini ya kocha mshikilizi Ryan Mason.

Fowadi na nahodha wa Spurs, Harry Kane alishuhudia mabao yake mawili yakikosa kuhesabiwa baada ya teknolojia ya VAR kubainisha kwamba alikuwa ameotea. Mbali na Kane, sogora mwingine wa Spurs aliyemshughulisha vilivyo kipa Illan Meslier wa Leeds ni beki Serge Aurier aliyepoteza nafasi nyingi za wazi.

Zikisalia mechi tatu pekee kwa kampeni za EPL msimu huu kutamatika rasmi, Spurs kwa sasa wanashikilia nafasi ya saba jedwalini kwa alama 56, saba nyuma ya Leicester City wanaofunga orodha ya nne-bora.

Leeds walioanza mechi hiyo dhidi ya Spurs wakishikilia nafasi ya 11, walipaa hadi nambari tisa baada ya kuwaruka Arsenal na Aston Villa watakaovaana na West Bromwich Albion na Manchester United mtawalia mnamo Mei 9, 2021.

Ushindi wa Leeds unamaanisha kwamba kikosi hicho cha kocha Marcelo Bielsa kitakamilisha kampeni za EPL msimu huu bila ya kushindwa nyumbani na timu yoyote miongoni mwa sita kuu kwenye EPL.

Kichapo kutoka kwa Leeds kilikuwa cha pili kwa Spurs kupokezwa hadi sasa tangu wamtimue kocha Jose Mourinho mnamo Aprili 19, 2021. Ina maana kwamba Spurs ambao wanapiga msimu wa 13 mfululizo bila taji lolote baada ya kupepetwa na Manchester City kwenye fainali ya Carabao Cup, sasa wako katika hatari ya kukosa kunogesha soka ya bara Ulaya muhula ujao.

Leeds watavaana na Burnley katika mchuao wao ujao wa EPL mnamo Jumamosi ya Mei 15 huku Spurs wakiwaalika Wolves siku moja baadaye.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Chungu cha Ionikos anayochezea Mkenya Abud Omar chakaribia...

Derby County ya kocha Wayne Rooney yaponea chupuchupu...