• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Lewandowski afungia Bayern Munich mabao matatu na kuvunja rekodi zaidi katika Bundesliga

Lewandowski afungia Bayern Munich mabao matatu na kuvunja rekodi zaidi katika Bundesliga

Na MASHIRIKA

ROBERT Lewandowski alifunga mabao matatu na kufikisha zaidi ya magoli 300 kambini mwa Bayern Munich katika mechi ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) iliyoshuhudia mabingwa hao watetezi wakichabanga Hertha Berlin 5-0 mnamo Jumamosi.

Lewandowski ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Poland, alitumia mechi hiyo kuvunja rekodi iliyowekwa na Gerd Muller mnamo 1970 kwa kufunga katika mechi yake ya 16 mfululizo ndani ya jezi za Bayern. Gerd alifunga mabao katika mechi 15 mfululizo. Wanaotaka kutuma ujumbe wao kumkumbuka wanaweza kutumia kiungo hiki: https://fcbayern.com/condolence-book-gerd/

Mabao mengine ya Bayern yalifumwa wavuni kupitia Thomas Muller na Jamal Musiala.

Ushindi huo uliosajiliwa na Bayern dhidi ya Hertha wanaokokota nanga mkiani mwa jedwali la Bundesliga uliwakweza masogora hao wa kocha Julian Nagelsmann hadi nafasi ya pili jedwalini nyuma ya viongozi Bayer Leverkusen wanaowazidi kwa idadi ya mabao.

Gerd Muller aliyeaga dunia mnamo Agosti 15 akiwa na umri wa miaka 75, alifunga mabao 547 kutokana na mechi 594 katika kipindi cha miaka 15 kambini mwa Bayern.

Lewandowski, 33, kwa sasa anajivunia kufunga mabao katika mechi 13 mfululizo za Bundesliga. Kwa upande wake, Thomas Muller sasa amefunga bao katika Bundesliga kwa misimu 13 mfululizo.

Bayern walijibwaga ugani kwa ajili ya mechi hiyo dhidi ya Hertha wakiwa na motisha ya kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi mnono wa 12-0 dhidi ya Bremer SV kwenye gozi la DFB Pokal German Cup mnamo Agosti 25, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Real Madrid wapiga Betis na kutua kileleni mwa jedwali la...

Juventus yapepetwa na Empoli nyumbani siku chache baada ya...