• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Lewandowski atuzwa kiatu cha dhahabu kwa kuibuka mfungaji bora katika ligi za bara Ulaya 2020-21

Lewandowski atuzwa kiatu cha dhahabu kwa kuibuka mfungaji bora katika ligi za bara Ulaya 2020-21

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Robert Lewandowski ametuzwa kiatu cha dhahabu cha soka ya bara Ulaya almaarufu European Golden Shoe baada ya kufungia Bayern Munich mabao 41 katika kampeni za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mnamo 2020-21.

Tuzo hiyo hutolewa kwa mfungaji bora zaidi katika ligi kuu zote za bara Ulaya.

Lewandowski, 33, ndiye mwanasoka wa pili anayesakata soka ya kulipwa nchini Ujerumani kuwahi kutia kapuni taji hilo baada ya aliyekuwa jagina wa soka kambini mwa Bayern, marehemu Gerd Muller (1971-72).

“Tuzo hii iwe ruzuku kwa watu wote ambao huwa kando yangu kila siku. Wote wanaonipiga jeki kitaaluma,” akasema nahodha huyo wa timu ya taifa ya Poland.

Idadi ya mabao yaliyofungwa na Lewandowski ligini mnamo 2020-21 ndiyo ya juu zaidi tangu Cristiano Ronaldo apokezwe taji hilo mnamo 2015 baada ya kufungia Real Madrid ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) jumla ya magoli 48.

Mnamo 2020-21, Lewandowski aliyechezeshwa mara 29 kwenye Bundesliga, alipiku Lionel Messi aliyefungia Barcelona mabao 30 katika La Liga pamoja na Ronaldo aliyepachikia Juventus ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) jumla ya magoli 29.

Tuzo hiyo imewahi kutwaliwa mara sita na Messi huku washindi wengine wa hivi karibuni wakiwa Ciro Immobile na Luis Suarez.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Waliosuka majonzi ya Wakenya mwaka 2018

Rais hajajadiliana na OKA kuhusu atakayerithi ikulu 2022...