• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Rais hajajadiliana na OKA kuhusu atakayerithi ikulu 2022 – Mudavadi

Rais hajajadiliana na OKA kuhusu atakayerithi ikulu 2022 – Mudavadi

Na SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi amekanusha madai kuwa Okoa Kenya Alliance (OKA) inafanya mikutano ya faragha na Rais Uhuru Kenyatta ili kupata mrithi wake mwaka ujao.

Muungano wa OKA unajumuisha Mabw Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetangula (Ford-Kenya) na kiongozi wa Kanum, Gedion Moi.

Tetesi zimekuwa zikihoji viongozi hao wamekuwa wakifanya mazungumzo na Rais Kenyatta kisiri, katika kile kinaonekana kama mchakato wa kusaka mrithi wake 2022.

Bw Mudavadi hata hivyo amekana madai hayo, akisema hayana msingi wowote.

Akifutilia mbali kauli ya Gavana wa Nyandarua Bw Francis Kimemia, ambaye ameibua mjadala kuwa ‘mtandao wa serikali’ ndio utaamua atakayemrithi Rais Kenyatta, Mudavadi amesema wapigakura ndio waamuzi wa atakeyeingia Ikulu.

“Wapigakura ndio wataamua atakayeingia Ikulu 2022,” akasisitiza kiongozi huyo wa ANC.

Bw Mudavadi na ambaye ametangaza nia yake kuwania kiti cha urais 2022 alisema hayo Jumanne usiku, kwenye mahojiano na runinga ya Citizen.

“Mjadala wa mtandao wa serikali kuamua atakayekuwa rais mwaka ujao hata haupaswi kutajwa wala kujadiliwa,” akasema.

Siku kadha zilizopita, Gavana wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru aliandikisha taarifa katika makao makuu ya Tume ya Maadili na Kupamabana na Ufisadi (EACC) kufuatia tetesi zinazomuandama za ufujaji fedha za kaunti na alikuwa ameandamana na mbunge wa Lugari, Bw Ayub Savula aliyedai ANC inamchumbia ili awe mgombea mwenza wa Mudavadi.

Bw Mudavadi amefutilia mbali kauli ya mbunge huyo ambaye ni naibu kiongozi wa ANC, akiitaja kama “matamshi binafsi yasiyowakilisha chama”.

“Hakuna tunayechumbia, japo tunaalika viongozi wenye maono na sera kama zetu kukomboa Kenya,” akaelezea.

You can share this post!

Lewandowski atuzwa kiatu cha dhahabu kwa kuibuka mfungaji...

QPR yaduwaza Everton kwenye Carabao Cup