• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Liverpool wapewa tena Real Madrid huku Bayern Munich wakivaana na PSG katika 16-bora UEFA

Liverpool wapewa tena Real Madrid huku Bayern Munich wakivaana na PSG katika 16-bora UEFA

NA MASHIRIKA

LIVERPOOL watavaana na mabingwa watetezi Real Madrid kwenye hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu – pambano litakalorejesha kumbukumbu za fainali ya kipute hicho mnamo 2021-22.

Real ambao ni washindi mara 14 wa taji la UEFA walikomoa Liverpool 1-0 katika fainali ya msimu jana iliyochezewa jijini Paris, Ufaransa.

Wafalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Manchester City, watakwaruzana na RB Leipzig ya Ujerumani huku Tottenham Hotspur wakionana na AC Milan ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Chelsea watamenyana na Borussia Dortmund huku Paris Saint-Germain (PSG) wakipewa Bayern. Droo hiyo itarejesha kumbukumbu za fainali ya 2019-20 ambapo Bayern walivuna ushindi wa 1-0 jijini Lisbon, Ureno.

Mechi za mkondo wa kwanza za hatua ya 16-bora zitasakatwa Februari 14-15 na 21-22 huku marudiano yakifanyika Machi 7-8 na 14-15.

Ni mara ya nne katika kipindi cha misimu sita ambapo Liverpool, wafalme mara sita wa UEFA, wamekutanishwa na Real kwenye kivumbi hicho. Miwili kati ya michuano hiyo, imekuwa ya fainali ambayo Real ilitamalaki mnamo 2017-18 na 2021-22.

Real ambao pia ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), walidengua Liverpool kwenye robo-fainali za UEFA mnamo 2020-21. Liverpool wametinga fainali ya UEFA mara tatu katika kipindi cha misimu mitano iliyopita.

Ni AC Milan (saba) na Real (14) pekee ndio wanajivunia mataji mengi zaidi ya UEFA kuliko masogora hao wa Jurgen Klopp. Mnamo 2018, Real walifunga Liverpool mabao 3-1 kwenye fainali ya UEFA na kunyanyua taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo.

Ingawa Man-City hawajawahi kutwaa taji la UEFA katika historia, wanapigiwa upatu wa kuibuka wafalme msimu huu. Walitinga fainali ya 2020-21 ila wakazidiwa ujanja na Chelsea waliowakung’uta 1-0 kabla ya Real kuwabandua kwenye nusu-fainali za 2021-22.

Washindani wao katika hatua ya 16-bora, Leipzig, walidenguliwa katika hatua ya makundi muhula jana na kwa sasa wanakamata nafasi ya sita kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Wafalme mara mbili wa UEFA, Chelsea, waliong’olewa na Real kwenye robo-fainali msimu uliopita. Dortmund ambao ni wapinzani wao katika raundi ya 16-bora hawajawahi kusonga mbele zaidi ya hatua ya robo-fainali tangu watinge fainali ya 2012-13 wakinolewa na kocha Jurgen Klopp ambaye sasa anadhibiti mikoba ya Liverpool.

Spurs waliopigwa na Liverpool 2-0 katika fainali ya UEFA 2018-19 jijini Madrid, watakutana na AC Milan kwa mara ya kwanza baada ya miaka 11. Droo hiyo itamshuhudia kocha Antonio Conte aliyenoa Inter Milan kati ya 2019 na 2021 akirejea Italia.

PSG ambao hawajapoteza mechi yoyote tangu Machi mwaka huu, wanasaka taji la UEFA kwa mara ya kwanza wakijivunia maarifa ya masupastaa Lionel Messi, Neymar na Kylian Mbappe. Napoli watavaana na Eintracht Frankfurt, Benfica wapimane ubabe na Club Bruges nao Inter Milan wamenyane na FC Porto.

DROO YA 16-BORA UEFA: 

RB Leipzig vs Man-City

Club Bruges vs Benfica

Liverpool vs Real Madrid

AC Milan vs Tottenham

Frankfurt vs Napoli

Dortmund vs Chelsea

Inter Milan vs Porto

PSG vs Bayern Munich

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Man-United kuvaana na Barcelona katika mchujo wa kuingia...

Youssoufa Moukoko aweka rekodi mpya ya ufungaji mabao...

T L