• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:44 PM
Liverpool watoka nyuma na kuendeleza masaibu ya Wolves katika EPL

Liverpool watoka nyuma na kuendeleza masaibu ya Wolves katika EPL

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL walifunga mabao mawili mwishoni mwa kipindi cha pili katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowashuhudia wakitoka nyuma na kupepeta Wolverhampton Wanderers 3-1 ugani Molineux.

Akinogesha mchuano wake wa 200 katika EPL, beki raia wa Scotland, Andy Robertson, aliwaweka Reds kifua mbele kunako dakika ya 85, dakika chache kabla ya Hugo Bueno wa Wolves kujifunga kutokana na kombora la Harvey Elliott.

Cody Gakpo alishirikiana vilivyo na Mohamed Salah mwanzoni ma kipindi cha pili na kusawazishia Liverpool waliojipata chini katika dakika ya saba Hwang Hee-Chan alipowaweka Wolves uongozini kupitia krosi ya Pedro Neto.

Ushindi huo uliwaweka Liverpool kileleni mwa jedwali kwa muda kabla ya michuano sita mingine ya EPL kusakatwa katika viwanja mbalimbali, Jumamosi.

Liverpool, ambao wamekuwa wa kwanza kufungwa na wapinzani kwenye mechi tatu kati ya tano zilizopita katika EPL msimu huu, sasa wanajivunia alama 13 huku pengo la pointi 10 likiwatenganisha na Wolves.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool walifungua kampeni zao za EPL muhula huu kwa sare ya 1-1 dhidi ya Chelsea kabla ya kukomoa Bournemouth (3-1), Newcastle (2-1) na Aston Villa (3-0) kwa usanjari huo.

Wolves sasa wamepoteza mechi nne kati ya tano zilizopita. Walianza muhula kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Manchester United kabla ya Brighton (4-1), kupiga Everton (1-0) na kukubali kichapo cha 3-2 kutoka kwa Crystal Palace.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Abiria 4 waaga dunia, tisa wajeruhiwa kwenye shambulio...

Wanaraga wa kike wa Kenya wapoteza vibaya dhidi ya Afrika...

T L