• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 7:55 PM
Liverpool yadengua Man-City FA

Liverpool yadengua Man-City FA

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL waliweka hai matumaini ya kujizolea mataji manne kwenye kampeni za msimu huu baada ya kukomoa Manchester City 3-2 ugani Wembley na kutinga fainali ya Kombe la FA.

Kusuasua kwa Man-City kuliwapa Liverpool nafasi ya kuwafunga mabao yote matatu katika kipindi cha kwanza kupitia kwa Ibrahima Konate na Sadio Mane aliyecheka na nyavu mara mbili.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool walinyanyua taji la Carabao Cup mwishoni mwa Februari 2022 na wanapigiwa upatu wa kukomoa Villarreal kwenye nusu-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Aidha, wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 73, moja pekee nyuma ya viongozi na mabingwa watetezi Man-City.

Man-City wanaonolewa na kocha Pep Guardiola, walikosa huduma za kiungo Kevin de Bruyne na beki Kyle Walker katika mchuano huo ulioshuhudia Zack Steffen akichukua nafasi ya kipa Ederson katikati ya michuma.

Man-City walirejea mchezoni katika kipindi cha pili na wakafunga bao la kwanza kupitia kwa Jack Grealish katika dakika ya 47 kabla ya Bernardo Silva kupachika la pili sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa.

Liverpool sasa watakutana na Chelsea au Crystal Palace kwenye fainali itakayochezewa ugani Wembley mnamo Mei 14, 2022.

Ushindi wa Liverpool unawaweka karibu na historia ya kuwa kikosi cha kwanza kutoka Uingereza kuwahi kunyanyua mataji manne katika msimu mmoja.

Kichapo kutoka kwa Liverpool kilizima matumaini ya Man-City kukamilisha kampeni za msimu huu wakijivunia mataji matatu kabatini. Miamba hao sasa wanatarajiwa kuelekeza makini yao kwenye kipute cha EPL na UEFA ambapo watakutana na Real Madrid kwenye mikondo miwili ya nusu-fainali.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ronaldo abeba Man-United dhidi ya Norwich City

Dortmund yadhalilisha Wolfsburg

T L