• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 6:55 PM
Lukaku aongoza Chelsea kuzamisha Arsenal katika gozi kali la EPL ugani Emirates

Lukaku aongoza Chelsea kuzamisha Arsenal katika gozi kali la EPL ugani Emirates

Na MASHIRIKA

ROMELU Lukaku alifunga bao lake la kwanza kambini mwa Chelsea – baada ya takriban miaka 10 tangu awajibikie kikosi hicho kwa mara ya kwanza – na kuongoza waajiri wake hao kupepeta Arsenal 2-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumapili ugani Emirates.

Lukaku ambaye aliwahi kuchezea Chelsea akiwa tineja, alipangwa katika kikosi cha kwanza dhidi ya Arsenal na huo ulikuwa mchuano wake wa kwanza ndani ya jezi za The Blues tangu asajiliwe kwa Sh15.2 bilioni kutoka Inter Milan ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Lukaku aliwatatiza pakubwa mabeki wa Arsenal huku akiwaweka Chelsea kifua mbele katika dakika ya 15 baada ya kushirikiana vilivyo na chipukizi Reece James aliyefunga goli la pili kutokana na krosi ya Mason Mount katika dakika ya 35.

Nusura Lukaku, 28, afungie Chelsea bao la tatu katika kipindi cha pili ila mpira wa kichwa alioelekeza langoni mwa wenyeji wao ulipanguliwa na kipa Bernd Leno.

Arsenal waliokosa huduma za beki Ben White kwa sababu ya corona, sasa wamepoteza debi nyingi za London kwenye kipute cha EPL kuliko jinsi walivyofanya msimu uliopita wa 2020-21 licha ya kwamba wamesakata michuano miwili pekee muhula huu.

Ni kwa mara ya tatu kwa Arsenal kupoteza mechi mbili za kwanza za msimu wa EPL na ni mara ya kwanza katika historia ya miaka 117 ya kuwepo kwa kikosi hicho kupoteza mechi hizo mbili za ufunguzi wa msimu bila kufunga bao.

Arsenal wanaonolewa na kocha Mikel Arteta walishuka dimbani wakitarajiwa kujinyanyua mbele ya mashabiki wao wa nyumbani baada ya kupepetwa 2-0 na limbukeni Brentford katika mechi ya kwanza msimu huu.

Ushindi wa Chelsea umewafanya mashabiki kuwapigia upatu wa kuwa wagombezi halisi wa taji la EPL msimu huu ikizingatiwa ukubwa wa kiwango cha ufufuo wa makali yao chini ya kocha Thomas Tuchel aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Frank Lampard mnamo Januari 2021.

Cha pekee ambacho Chelsea walikosa msimu uliopita wa 2020-21 ni fowadi wembe wa kufunga mabao kirahisi. Hata hivyo, walifaulu kukamilisha kampeni za EPL katika nafasi ya nne na kujinyanyulia ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (Uefa) wakijivunia huduma za mvamizi Timo Werner aliyeshirikiana na Olivier Giroud pamoja na Tammy Abraham ambao kwa sasa wameyoyomea Italia kuchezea AC Milan na AS Roma mtawalia.

Siku tano kabla ya kujaza miaka 10 tangu achezee Chelsea kwa mara ya kwanza, mechi dhidi ya Arsenal ilikuwa ya 16 kwa Lukaku kuwajibikia The Blues. Nyota huyo raia wa Ubelgiji amewahi pia kuchezea West Bromwich Albion, Everton, Manchester United na Inter Milan.

Chelsea wangalifunga mabao zaidi kupitia Kai Havertz na Lukaku aliyeelekezea Arsenal makombora manane kati ya 22 ambayo waajiri wake walimvurumishia kipa Leno.

Hofu zaidi kwa wapinzani wakuu wa Chelsea kwa sasa ni namna ya kukabiliana na uthabiti wa kikosi hicho kinachojivunia pia viungo matata kama vile N’Golo Kante na Jorginho.

Kibarua kijacho cha Chelsea kitakuwa dhidi ya Liverpool ugani Anfield mnamo Agosti 28, 2021. Chini ya mkufunzi Jurgen Klopp, Liverpool pia watajibwaga ulingoni wakijivunia rekodi nzuri ya kushinda mechi mbili za kwanza msimu huu dhidi ya Norwich City (3-0) na Burnley (2-0).

Mbali na White aliyesajiliwa kwa Sh7.8 bilioni kutoka Brighton, Arsenal walikosa huduma za wanasoka mahiri Alexandre Lacazette na Pierre-Emerick Aubameyang wanaougua.

Ingawa hivyo, dalili zote zinaashiria kwamba Arsenal watakuwa tena na wakati mgumu msimu huu baada ya kufunga misimu miwili iliyopita ya kampeni za EPL katika nafasi ya nane jedwalini.

Agosti 1992 ndio ulikuwa mwezi wa kwanza wa kipute cha EPL. Hiyo ndiyo mara ya mwisho kabla ya sasa kwa Arsenal kujipata ndani ya mduara wa vikosi vinavyokodolea macho hatari ya kuteremshwa ngazi hadi Ligi ya Daraja ya Kwanza (Championship) baada ya mechi mbili za kwanza za msimu kusakatwa.

Arsenal wameratibiwa kuvaana na West Brom katika mchuano ujao katika EFL Cup mnamo Agosti 25 kabla ya kuwaendea mabingwa watetezi Man-City ligini mnamo Agosti 29, 2021 ugani Etihad.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

WARUI: Serikali iharakishe maandalizi ya sekondari kwa CBC

Ronaldo aachwa nje ya kikosi cha kwanza cha Juventus tetesi...