• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Madrid wapigwa breki na Sociedad

Madrid wapigwa breki na Sociedad

Na MASHIRIKA

REAL Madrid walipoteza fursa ya kuwaruka Barcelona na kuwakaribia Atletico Madrid kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Jumatatu usiku baada ya kulazimishiwa sare ya 1-1 kutoka kwa Real Sociedad uwanjani Alfredo Di Stefano.

Licha ya kutamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira, Real walipoteza nafasi nyingi za wazi kupitia kwa Mariano Diaz Mejia na Raphael Varane walioshuhudia makombora yao yakibusu mwamba wa lango la Sociedad.

Sociedad ndio waliokuwa wa kwanza kucheka na nyavu za wenyeji wao kupitia fowadi Portugues Manzanera aliyeshirikiana vilivyo na beki wa zamani wa Arsenal, Nacho Monreal.

Vinicius Jr aliyeingia uwanjani katika dakika ya 61 ndiye aliokoa chombo cha kocha Zinedine Zidane kwa kufungia waajiri wake Real bao la kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili.

Mchuano huo ulikuwa wa 100 kwa Vinicius ambaye ni chipukizi raia wa Brazil mwenye umri wa miaka 20 kuchezea Real. Goli alilofunga lilikuwa zao la ushirikiano kati yake na beki Lucas Vazquez.

Sare hiyo ilipiga breki rekodi nzuri ya Real ambao walijibwaga ugani wakijivunia kushinda msururu wa mechi tano katika mashindano yote.

Sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 53 sawa na Barcelona wanaowazidi kwa idadi ya magoli. Atletico wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa pointi 58 na nafuu zaidi kwao ni kwamba wana mechi moja zaidi ya kusakata ili kufikia idadi ya michuano ambayo imepigwa na washindani wao wakuu wakiwemo Sevilla wanaofunga mduara wa nne-bora kwa pointi 48. Sociedad wanakamata nafasi ya tano kwa alama 42.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

ReplyForward
  • Tags

You can share this post!

Wasichana mitaani waonywa dhidi ya ndoa za mapema

Jeraha kumnyima kigogo Ibrahimovic fursa ya kucheza dhidi...