• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:10 PM
Man-City wafungua mwanya wa alama sita kileleni mwa jedwali la EPL baada ya kukomoa Leicester

Man-City wafungua mwanya wa alama sita kileleni mwa jedwali la EPL baada ya kukomoa Leicester

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walihimili ushindani mkali kutoka kwa Leicester City katika kipindi cha pili na kuwakomoa wageni wao 6-3 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumapili uwanjani Etihad.

Mechi hiyo ilikuwa ya tisa mfululizo kwa mabingwa hao watetezi wa EPL kusajili ligini msimu huu na sasa wanajivunia pengo la alama sita kati yao na nambari mbili Liverpool kileleni mwa jedwali.

Man-City walianza mechi hiyo kwa matao ya juu na wakachukua uongozi wa 4-0 kufikia dakika ya 25 kutokana na magoli ya Kevin de Bruyne na Ilkay Gundogan pamoja na penalti za Riyad Mahrez na Raheem Sterling.

Hata hivyo, Leicester walianza kipindi cha pili kwa makali zaidi na wakapachika wavuni magoli matatu ya haraka chini ya dakika ya 10 kupitia kwa James Maddison, Ademola Lookman na Kelechi Iheanacho waliofanya mambo kuwa 4-3.

Ingawa matokeo hayo yaliwapa Leicester matumaini ya kurejea mchezoni na hata kuondoka ugani Etihad na alama moja au tatu, chombo chao kilizamishwa kabisa na Aymeric Laporte na Sterling waliofungia Man-City katika dakika za 69 na 87 mtawalia.

Kwa kuwa mechi iliyokuwa ikutanishe Liverpool na Leeds United iliahirishwa kwa sababu ya janga la corona, masogora wa kocha Pep Guardiola walikuwa na kiu ya kufungua mwanya mkubwa wa alama kati yao na washindani wao wakuu.

Liverpool kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 41 sawa na Chelsea waliokung’uta Aston Villa 3-1 ugani Villa Park. Leicester wanakamata nafasi ya 10 kwa alama 22 sawa na Villa.

Bao ambalo De Bruyne alifungia Man-City lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Fernandinho. Mahrez alipachika wavuni goli la pili kupitia penalti iliyotokana na tukio la Youri Tielemans kumchezea visivyo beki Laporte. Masihara ya kipa Kasper Schmeichel aliyeshindwa kudhibiti krosi ya Joao Cancelo yalichangia bao la tatu ambalo Man-City wlaifungiwa na Gundogan kabla ya Sterling kufunga la nne kupitia penalti baada ya Tielemans kumwangusha ndani ya kijisanduku.

Man-City walijibwaga ugani kwa ajili ya mechi dhidi ya Leicester wakijivunia kufunga mabao 24, ukiwemo ushindi mnono wa 7-0 dhidi ya Leeds United.

Hata hivyo, ambacho hakikutarajiwa ni jinsi Leicester walivyojibu mapigo ya wenyeji wao katika kipindi cha kwanza kwa kufunga mabao matatu ya haraka mwanzoni kwa kipindi cha pili licha ya kukosa huduma za wanasoka wengi wa haiba kubwa kutokana na majeraha.

Mabao matatu ambayo Man-City walifungwa na Leicester chini ya dakika 10 za kipindi cha pili yaliwiana na idadi ya magoli ambayo miamba hao walikuwa wamefungwa katika mechi nane za awali ligini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Martial asema huu ndio wakati mwafaka zaidi kwake kuondoka...

West Ham wateremka zaidi katika jedwali la EPL baada ya...

T L