• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Man-United padogo kuaga Europa League baada ya AC Milan kuwalazimishia sare ya 1-1 katika mkondo wa kwanza Old Trafford

Man-United padogo kuaga Europa League baada ya AC Milan kuwalazimishia sare ya 1-1 katika mkondo wa kwanza Old Trafford

Na MASHIRIKA

UTEPETEVU wa mabeki wa Manchester United uliruhusu AC Milan ya Italia kutoka nyuma na kuwalazimishia sare ya 1-1 kwenye mchuano wa mkondo wa kwanza wa Europa League uliochezewa uwanjani Old Trafford mnamo MACHI 11, 2021.

Sajili mpya Amad Diallo aliwaweka Man-United kifua mbele kunako dakika ya 50 katika tukio lililotarajiwa kuwapa masogora hao wa kocha Ole Gunnar Solskjaer ushindi muhimu katika gozi hilo.

Hata hivyo, Milan walisawazishiwa katika dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza kupitia kwa Simon Kjaer aliyemzidi ujanja beki Nemanja Matic kabla ya kumwacha hoi kipa Dean Henderson.

Awali, Milan wanaonolewa na kocha Stefano Pioli, walishuhudia bao walilofungiwa na Franck Kessie katika kipindi cha kwanza likifutiliwa mbali na VAR kwa madai kwamba fowadi huyo alitikisa nyavu baada ya kunawa mpira.

Milan walishuka dimbani bila ya kujivunia huduma za fowadi matata Zlatan Ibrahimovic anayeuguza jeraha la mguu.

Kwa upande wake, bao la Amad lilikuwa lake la kwanza katika mchuano wa tatu akivalia jezi za Man-United. Goli lililopachikwa wavuni na mshambuliaji huyo raia wa Ivory Coast lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na kiungo raia wa Ureno, Bruno Fernandes.

Mchezaji mwingine aliyetatiza pakubwa mabeki wa Milan kwa upande wa Man-United ni Anthony Martial aliyemshughulisha vilivyo kipa Gianluigi Donnarumma.

Milan kwa sasa wanatarajiwa kuvaana na Man-United katika mchuano wa marudiano utakaowakutanisha uwanjani San Siro, Italia mnamo Machi 18, 2021. Miamba hao wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) watajibwaga katika uga wao wa nyumbani wakihitaji angalau sare tasa au ushindi wa aina yoyote ili kutinga hatua ya robo-fainali za Europa League muhula huu wa 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Hofu idadi ya visa vipya vya Covid-19 ikiendelea kupanda

Vipusa wa Man-City wakomoa Fiorentina 8-0 na kufuzu kwa...