• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Man-United wawasilishia Chelsea ofa ya tatu kwa ajili ya kumsajili Mason Mount

Man-United wawasilishia Chelsea ofa ya tatu kwa ajili ya kumsajili Mason Mount

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United wametoa ofa mpya ya Sh9.8 bilioni ambayo sasa ni ya tatu kwa ajili ya kumsajili kiungo mzoefu wa Chelsea, Mason Mount.

Mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wametishia kujiondoa kwenye mbio za kujitwalia maarifa ya Mount iwapo jaribio lao la tatu kumshawishi kiungo huyo raia wa Uingereza litakataliwa na Chelsea.

Inaarifiwa kwamba Chelsea wanataka yeyote anayemezea mate huduma za Mount kuweka mezani kima cha Sh12.5 bilioni.

Hata hivyo, Man-United wanahisi kwamba ada hiyo inayotakiwa na Chelsea ni ya juu sana ikizingatiwa kwamba Mount amesalia na mwaka mmoja pekee kwenye mkataba wake wa sasa ugani Stamford Bridge.

Man-United tayari wameshuhudia ofa zao za awali za Sh7.1 bilioni na Sh8.9 bilioni kwa ajili ya Mount zikikataliwa na Chelsea.

Kocha wa Man-United, Erik ten Hag anataka Mount awe sajili wake wa kwanza muhula huu kadri anavyopania kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya kampeni za muhula ujao hasa katika soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Maafikiano ya kibifasi si tatizo kwa kuwa Man-United wana hakika kwamba Mount anatamani pia kutua ugani Old Trafford na kuanza kuvalia jezi zao.

Mount amefunga mabao 33 kutokana na mechi 195 ambazo amechezea Chelsea tangu 2019. Alikosa idadi kubwa ya mechi za mwisho wa msimu huu wa 2022-23 kutokana na jeraha huku Chelsea wakiambulia nafasi ya 12 jedwalini – nafasi ya chini zaidi kwa kikosi hicho kuwahi kukamata katika kipindi cha miaka 25.

Alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshindia Chelsea taji la UEFA mnamo 2021 na akaanza mechi hiyo iliyowashuhudia wakitandika Manchester City 1-0. Aidha, aliongoza Chelsea kushinda Kombe la Klabu Bingwa Duniani na Uefa Super Cup.

Mount, 24, amechezea Uingereza mara 36 na amefunga mabao matano huku akiwa sehemu ya kikosi kilichowajibishwa na kocha Gareth Southgate kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Mount alipokea malezi ya soka katika akademia ya Chelsea kabla ya kujiunga na Vitesse ya Uholanzi kwa mkopo mnamo 2017-18 ambapo alifunga mabao tisa kutokana na mechi 29 za Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie).

Msimu uliofuata, alitumwa kambini mwa Derby County kwa mkopo ambapo alipachika wavuni mabao manane kutokana na mechi 35 za Ligi ya Daraja ya Kwanza (Championship) chini ya kocha Frank Lampard. Derby County almaarufu Rams walipigwa 2-1 na Aston Villa kwenye mchujo wa kufuzu kwa soka ya EPL.

Baada ya kurejea kambini mwa Chelsea mnamo 2019, Mount alipata uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza chini ya kocha Lampard aliyemtegemea sana ugani Stamford Bridge.

Mnamo Mei 2023, Chelsea walimpokeza kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino, mikoba yao ya ukufunzi huku akijaza nafasi ya Lampard aliyechukua nafasi ya Graham Potter aliyepigwa kalamu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Olimpiki Maalum: Lynette Gitimu na Abigail Njuguna wavunia...

Mtindo wa wahalifu kurudia makosa waendelee kufurahia...

T L