• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Markstam Orwa asema bidii inaweza kumfikisha kwa viwango vya CR7

Markstam Orwa asema bidii inaweza kumfikisha kwa viwango vya CR7

NA PATRICK KILAVUKA

WINGA Markstam Orwa ni kifaa cha kuotea mbali na anaamini kwamba, siku za majaliwa anaweza kufuata kisawasawa nyayo za staa Cristiano Ronaldo wa Ureno ambaye anachezea klabu ya Al-Nasr. 

Anakariri kwambla, anajizatiti sasa kujiundia nafasi yake katika ulimwengu wa soka akifuata unyounyo hulka ya mchezaji mahiri na mtajika huyo.

Mwanasoka Orwa kwa sasa anafukuzia chatu cha dhahabu katika Ligi ya Kanda, FKF, Nairobi (NWRL) akiwa katika timu ya Ligi Ndogo ambayo inapatikana mkabala wa barabara wa Ngong, Nairobi.

Kufikia sasa makala yanapoandikwa, amecheka na nyavu mara sita.

Winga Markstam Orwa akingangana kujinyanyua baada ya kuchezewa visivyo. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Mwanadimba Orwa, alianza kucheza soka akiwa na miaka minane akiwa darasa la pili shule ya msingi ya Gilgili Hill Academy, Nakuru kabla kuchezea shule ya sekondari ya Kangumo High, Kaunti ya Nyeri.

Anasema ni akiwa Kangumo, kipaji chake cha soka kilinawiri sana kwani, huu ndio wakati alikuwa ameanza kujikuza kisoka na kujua zaidi mbichi na mbivu akidhamiria kuwa msakataji wa kabumbu hodari.

Alishirikiana na wenzake katika shule ya upili kufika katika nusu fainali ya Michezo ya Shule za Upili za Kaunti Nyeri na alitazawzwa mchezaji bora katika ngarambe hiyo.

Vile vile alituzwa mchezaji bora katika patashika ya Under 13 Eastlands, Nairobi.

Kwa minajili ya kujiendeleza kisoka baada ya kuhitimisha masomo ya sekondari, alifurahia kupata nafasi ya kujichonga zaidi katika akademia ya soka ya Ligi Ndogo mwaka 2022 na bila hili wala lile, alipewa nafasi katika kikosi cha kwanza kwani kipawa si cha kuficha!

Chini ya mkuzi wa kipaji chake kambini Ligi Ndogo Academy Florence Adhiambo, winga Orwa anasema anazidi kuona akitanuka kwani, amepata jukwaa la kujikwatua kisoka.

Anadokeza kwamba mkuzi huyo, amemhimiza kujikakamua zaidi kuhakikisha halegezi kamba kuivuta kamba yake ya kandanda hadi achezee timu tajika nchini kabla kufikiria kutoa huduma zake ughaibuni.

Winga Markstam Orwa akiwa na wengine wakisherekea bao alilofunga dhidi ya Kangemi Atletico uwanjani Kihumbuini. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Mchezaji wa pembeni Markstam ni shabiki sugu wa timu ya Arsenal. Anasema hiyo ndiyo timu ambayo inalandana na mfumo aupendao wa mchezo na majaliwa akipata nafasi ya kuicheza ughaibuni atahiari kuisakatia.

Hata hivyo, hapa nchini anasema mtima wake waihusudu Gor Mahia licha ya kuwa mabingwa mara 19 katika soka ya Kenya, wamewagubia wachezaji kuimarisha timu kila wakati.

Markstam anafichua kwamba mazoezi yamekuwa kiungo cha kutoa ubutu wa kipaji na kupata uzoefu zaidi. Isitoshe, kuzingatia mawaidha ya kocha yamekuwa yakinogesha uchezaji wake na kujiongezea imani na matumaini kwamba, safari yake ya soka iko katika mkondo wa kufikia ufanisi.

  • Tags

You can share this post!

Chepng’etich kivutio Istanbul Half Marathon nchini...

Miti 20,000 kupandwa kando ya bwawa la Karimenu II Gatundu

T L