• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 1:16 PM
Mashemeji Derby yaishia sare Nairobi City Stars ikigomea Bandari Mombasa

Mashemeji Derby yaishia sare Nairobi City Stars ikigomea Bandari Mombasa

CECIL ODONGO Na ABDULRAHMAN SHERIFF

MABINGWA wa zamani AFC Leopards na Gor Mahia wameagana sare tasa katika mechi kali ya Debi ya Mashemeji ugani Nyayo, Nairobi, Jumapili.

Mchuano huo ambao ulikuwa wa KPL ulishudhuriwa na halaiki ya mashabiki kutoka timu zote mbili.

Pwani mwa nchi, wachezaji wa Nairobi City Stars walikataa kuendelea na mchezo kipindi cha pili baada ya Bandari kufunga bao la pili timu hizo zikiwa zimekabana koo ya 1-1.

Sare dhidi ya Ingwe ilisongesha K’Ogalo hadi nafasi ya tatu kwa alama 24 baada ya mechi 11, japo vigogo hao bado wana mechi mbili kiporo.

Kwa upande mwingine, AFC wako namba nane kwa alama 18, sawa na Kenya Police ila wanadunishwa na uchache wa mabao.

Hii ilikuwa debi ya 95 kati ya Gor na AFC; K’Ogalo imeshinda mara 34, Ingwe mara 28 huku mechi 33 zikiishia sare.

Mechi hiyo iliwania kwa karibu na timu zote ila Ingwe wana kila sababu ya kujilaumu kwa kukosa nafasi kadhaa za kufunga hasa robo ya mwisho ya mtanange.

“Tuliwalemea Gor na kwa mtazamo wangu tungeshinda iwapo tungetumia nafasi zetu,” akasema kocha wa AFC raia wa Ubelgiji Patrick Aussems.

“Ni alama ambayo tumepigania na inastahili ila ukweli ni kuwa tulicheza vizuri dhidi ya Gor na ukizingatia baadhi ya nafasi ambazo tulizikosa, nashawishika kusema tungeenda nyumbani na alama zote tatu,” akaongeza

Mwenzake wa Gor, Johnathan McKinstry, alikubali kuwa mara hii walilemewa na akaridhika na sare.

“Ni matokeo ya kuwastani japo nafasi za kufunga ziliadimika kwa timu zote mbili. Leopards walikuwa juu hasa dakika 15 za mwisho na tulinusurika mikononi mwao. Nashukuru kwa hii alama moja,” akasema Kocha huyo raia wa Ireland ya Kaskazini.

Makocha wote walishukuru mashabiki kwa kujitokeza kwa wingi katika mechi hiyo wakisema hiyo ni ishara nzuri kwa soka ya Kenya imepiga hatua.

Kule Mombasa, maafisa wa City Stars waliingia uwanjani kupinga uamuzi wa refarii wa kukubali bao la mkwaju wa penalti lililofungwa na Willam Wadri baada ya Umaru Kasumba kuangushwa chini kutokana na mpira wa kona.

Bandari ilikuwa imechukua uongozi kwenye dakika ya 36 Abdalla Hassan alipopokea pasi safi kutoka kwa James Kinyuma na kutuma kombora hadi wavuni.

Hata hivyo, wageni hao kutoka Nairobi walisawazisha kunako dakika ya 45 kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Ezekiel Odera.

Bandari ilijipatia bao la pili dakika za majeruhi mfungaji akiwa Wadri.

Bao hilo ndilo liliwafanya maafisa pamoja na wachezaji kugoma kuendelea kucheza.

Hivyo, hivyo baada ya dakika kadhaa refa akapuliza kipenga cha kuvunja mechi.

  • Tags

You can share this post!

Serikali kusaka wanaorai wasichana wa shule kushiriki...

Ruto kufungua semina ya Bunge la Kitaifa na Muungano wa CPA...

T L