• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:15 PM
Mshukiwa wa ujambazi auawa kwa kupigwa risasi na polisi Mukuru-Mariguini

Mshukiwa wa ujambazi auawa kwa kupigwa risasi na polisi Mukuru-Mariguini

Na SAMMY KIMATU

MAAFISA wa polisi walimpiga risasi na kumuua mshukiwa mmoja wa ujambazi katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Mariguini, South B katika kaunti ndogo ya Nairobi.

Katika kisa hicho cha saa kumi na mbili za jioni, washukiwa wengine wawili walifanikiwa kutoroka huku msako mkali wa kuwatafuta ukianzishwa.

Akithibitisha kisa hicho, mkuu wa polisi eneo la Makadara, Bw Timon Odingo alisema mshukiwa aliyekuwa na bastola ni miongoni mwa waliotoroka.

“Washukiwa walikuwa wanaume watatu mtaani humo. Wakazi walipowaona washukiwa wakiwa na wasiwasi huku wakiliona bastola ikichomoka chini ya nguo yake, walipigia polisi simu. Maafisa wangu waliovalia kiraia waliweka mtego na kuzingira mtaa huo,” Bw Odingo akasema.

Vilevile, Bw Odingo aliongeza kwamba wahalifu walipofika katika eneo la kuoshea magari na kuuzia makaa, walishtuka kuwapata maafisa wetu njiani.

“Mmoja wao alichomoa bastola yake na kupiga risasi juu hewani ili kuwashtua watu barabarani. Polisi walikuwa wepesi kujibu na ndipo mshukiwa akapigwa risasi na kuuawa papo hapo. Wenzake walifanikiwa kutorokea mtaani japo tumeanzisha msako kuona wametiwa baroni,” Bw Odingo akaambia wanahabari.

Vilevile, polisi wanashuku washukiwa walikuwa na mpango wa kufanya uhalifu pahali pasipojulikana au wawe walikuwa wakienda kukodisha bastola waliyokuwa nayo.

Kisa hicho liliwavutia wananchi wengi na kusababisha msongamano wa magari kwenye barabara zilizoko South B na Eneo la Viwandani kwani wafanyakazi wengi walikuwa wakitoka kazini.

Kufikia usiku, maafisa wa polisi walionekana wakiwa wengi katika mitaa ya mabanda katika tarafa hiyo wakiwasaka majambazi waliotoroka.

“Polisi walikuwa wengi usiku ndani ya mitaa ya mabanda huku South B sawia na barabarani huku wasiwasi ukitanda watu wakiongopa kukamatwa katika kukurukakara za msako wa polisi,” Mmiliki wa kioski mtaani Mariguini ambaye aliogopa kujitambulisha akasema.

Jumatano, serikali kupitia kwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i ilisema usalama umethibitiwa vilivyo msimu wa sherehe huku maafisa wote wa polisi walio likizoni wakiamriwa kurudi kazini.

“Kila mkenya amehakikishiwa usala wa kutosha tunapoelekea, wakati na baada ya sherehe za Krisimasi na Mwaka Mpya,’ Bw Matiang’i akatangaza.

You can share this post!

Mathare North All Stars na Kapsambo waibuka mabingwa NCFA

Kinda Caleb Atuta ajisuka akilenga kufikia viwango vya CR7

T L