• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Misri wamtimua kocha Ehab Galal baada ya kusimamia mechi tatu pekee

Misri wamtimua kocha Ehab Galal baada ya kusimamia mechi tatu pekee

Na MASHIRIKA

SHIRIKISHO la Soka la Misri (EFA ) limemfuta kaza kocha Ehab Galal baada ya kusimamia mechi tatu pekee za timu ya taifa.

Galal, 54, alijaza nafasi ya Carlos Queiroz mnamo Aprili 2022 baada ya Misri almaarufu ‘The Pharaohs’ kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Kutimuliwa kwa Galal kulichochewa na kichapo cha 2-0 ambacho Misri walipokezwa na Ethiopia katika mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2023 kabla ya Korea Kusini kuwapepeta 4-1 kirafiki.

Kwa mujibu wa Hazem Emam ambaye ni mwanachama wa bodi ya usimamizi wa EFA, shirikisho hilo kwa sasa linasaka huduma za kocha mpya kutoka ughaibuni.

Galal aliteuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Misri baada ya kuhudumu kwa msimu mmoja kambini mwa kikosi cha Pyramids jijini Cairo. Aliwahi pia kuwatia makali masogora wa klabu za Zamalek, El Masry na Al Ahly Tripoli.

Katika mchuano wake wa kwanza kabisa akidhibiti mikoba ya Misri mnamo Juni 2022, masogora wake walisubiri hadi dakika za mwisho wa mchezo ili kupiga Guinea 1-0 katika mechi ya kufuzu kwa AFCON 2023.

Hata hivyo, mechi mbili zilizopotezwa na Misri bila kujivunia huduma za nahodha wao Mohamed Salah ambaye ni fowadi matata wa Liverpool, zilichangia kufurushwa kwa Galal.

Queiroz ambaye ni kocha wa zamani wa Ureno na Iran, aliwahi kuwa msaidizi wa Sir Alex Ferguson kambini mwa Manchester United. Aliongoza Misri ambao ni mabingwa mara saba wa AFCON kutinga fainali ya kipute hicho mnamo Februari 2022 nchini Cameroon kabla ya Senegal kuwakomoa kwa penalti 4-2.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

LISHE: Chagua chakula cha kuzuia matatizo ya kiafya

Wachezaji 10 wa EPL katika orodha ya chipukizi 100...

T L