• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 2:00 PM
Mwitaliano Jacobs apongeza Omanyala baada ya kulemewa

Mwitaliano Jacobs apongeza Omanyala baada ya kulemewa

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa dunia mbio za mita 60 na Olimpiki 100m Marcell Jacobs mnamo Alhamisi amepongeza Ferdinand Omanyala baada ya mfalme huyo wa Afrika na Jumuiya ya Madola mbio za 100 katika fainali ya 60m kumuonyesha kivumbi kwenye riadha za ukumbini za Hauts-de-France Pas-de-Calais mjini Lievin, Ufaransa.

Omanyala ameshiriki mashindano manne nchini Ufaransa.

Afisa huyo wa polisi ameshinda mbio sita za mita 60 ikiwemo kumduwaza Jacobs kutoka Italia, na kumaliza mara mbili katika nafasi ya pili.

Omanyala, 27, alianza msimu kwa kukamilisha 60m kwa sekunde 6.66 katika makundi mjini Miramas na kukamata raundi hiyo nambari mbili kwa 6.60 nyuma ya raia wa Ivory Coast, Arthur Cisse.

Bingwa huyo wa Kipchoge Keino Classic 2022 kisha alikamata nafasi ya pili nyuma ya Cisse katika raundi ya Mondeville makundini kwa 6.63 kabla ya kulipiza kisasi katika fainali alipobeba taji kwa rekodi ya kitaifa ya 6.55. Alikimbia 6.61 makundini na 6.56 mjini Paris kabla ya kufunga msimu kwa rekodi mpya ya kitaifa 6.54 mjini Lievin alikobwaga Mwitaliano Jacobs. Omanyala alikuwa amekimbia 6.58 makundini.

Jacobs amekubali kushindwa akisema: “Mtu pia hujifunza kutokana na kupoteza, si mara yangu ya kwanza. Inauma kumaliza katika nafasi ya pili. Kuanzia kesho (Februari 17), nitazamia mazoezi na kurekebisha vitu ninavyostahili kurekebisha. Nataka kukabiliana na majukumu yajayo nikiwa sawa kabisa. Hongera @ferdiomanyala. Tuonane hivi karibuni,” Jacobs alisema kupitia mtandao wake wa Twitter.

Omanyala ameshukuru Mungu kwa msimu mzuri.

“Ninapofika mwisho wa kampeni ya kufana ya riadha za ukumbini, nataka kushukuru Mungu kwa afya njema. Pia, nashukuru timu yangu ya A kwa kufanya uamuzi wa kushindana katika riadha za ukumbini mwisho wa mwaka 2022, na kuhakikisha niko tayari. Umekuwa msimu mzuri. Kwa mashabiki wangu wote duniani na hasa nchini Kenya, shukran kwa usaidizi wenu. Kila mmoja wenu ni muhimu. Asanteni sana,” amesema Omanyala mnamo Februari 16.

Omanyala atashiriki mbio zake za kwanza za 100m uwanjani mnamo Februari 24-25 ugani Nyayo, Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

Wanajeshi wa KDF waua Al-Shabaab watatu, wafanikiwa kupata...

Matumizi mbalimbali ya mafuta ya haradali

T L