• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Namwamba awatuza wanahabari kwenye hafla ya kufana

Namwamba awatuza wanahabari kwenye hafla ya kufana

NA TOTO AREGE

HISTORIA imewekwa Jumatano wakati Waziri wa Michezo Ababu Namwamba amewatuza wanahabari 195 wa michezo kwa mara ya kwanza kabisa.

Hafla hiyo imeandaliwa katika hoteli ya Weston jijini Nairobi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw Namwamba amewatunuku wanahabari 195 wa michezo na watengenezaji wa video za kupakiwa kwenye majukwaa mbalimbali mtandaoni.

“Katika kila mfanyalo, fanyeni kwa uwezo wenu. Inafaa tutambue juhudi za watu ambao wanaletea Kenya fahari kubwa. Tuna tabia mbaya ya kuwasifia watu hawa baada ya kuaga dunia. Wakifa tu, tunajitokeza kwa wingi kuwasifia, hata tunavaa vizuri na kuwavalisha vizuri hata wakifa,” akasema Bw Namwamba.

Wakati huo huo, serikali sasa itatuza wanamichezo bora na watengenezaji wa video za mitandaoni kila mwaka.

Amesema wanariadha na watengenezaji wa video za kupakiwa kwenye majukwaa mtandaoni ndio mabalozi bora wa nchi na hivyo tunahitaji kuwaheshimu vyema.

Wakati wa hafla ya utoaji tuzo, Bw Namwamba amethibitisha kujitolea kwa wizara yake kuhakikisha wanahabari wa michezo na sanaa ya ubunifu wanafanya kazi zao kwa weledi na kupata usaidizi wa serikali.

Hafla ya kwanza ya kuwatuza wanamichezo nchini ilifanyika Julai 29 katika hoteli ya Safari Park jijini Nairobi. Ilileta pamoja takriban wanaspoti 1,200 na watengenezaji wa video za kupakiwa katika majukwaa ya mtandaoni.

Wanahabari hao wametunukiwa vikombe na kwa pamoja wamepokezwa hundi ya Sh5 milioni, pesa ambazo watagawana.

Rais wa Chama cha Wanahabari wa Michezo nchini (SJAK) James Waindi, amempongeza Bw Namwamba kwa kuwatunuku wanahabari hao.

“Hatujawahi kutambuliwa na kutuzwa, hili ni jambo kubwa kwetu. Kila timu ya Taifa inapotoka kuwakilisha taifa, tunaomba tupate angalau nafasi moja au mbili na tutaiwakilisha nchi vizuri. Pia kuna tuzo za Gala mwishoni mwa mwaka huu na natumai utatuunga mkono,” alisema Waindi.

Bw Waindi amemuahidi waziri kwamba watafanya kazi kwa ushirikiano.

  • Tags

You can share this post!

Walinzi wa Fernandes Barasa watiwa mbaroni kwa kushambulia...

Makali Mulu ndiye mkali wao kwa kushiriki mijadala Bungeni

T L