• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 12:25 PM
Walinzi wa Fernandes Barasa watiwa mbaroni kwa kushambulia DCI

Walinzi wa Fernandes Barasa watiwa mbaroni kwa kushambulia DCI

NA MWANGI MUIRURI 

WALINZI watatu na dereva wa Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa wametiwa nguvuni baada ya kushambulia afisa mkuu wa Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) wa kaunti ndogo ya Luanda.

Walinzi hao ambao ni maafisa wa polisi walinaswa Jumanne mwendo wa saa moja jioni na kwa sasa wamefungiwa katika kituo cha polisi cha Luanda wakisubiri kufikishwa mahakamani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Inspekta Jenerali wa Polisi Bw Japhet Koome, maafisa hao ni Konstebo 99512 Edwin Juma anayehudumia kituo cha polisi cha Harambee, Kakamega, ambaye alikuwa anejihami kwa bunduki aina ya Jericho usajili ukiwa ni KE-KP 45302268 pamoja na risasi 15.

Wa pili ni Konstebo 244633 jina likiwa ni Jacob Wamalwa wa kituo cha polisi cha Central mjini Kakamega akiwa na bunduki aina ya Ceska iliyo na usajili PC KE-KP-G6008 na risasi 15.

Aidha, Konstebo Duncan Ogweno, nambari ya kikosi ikiwa ni 240604 wa kituo cha polisi cha Central aliyekuwa amejihami kwa bunduki aina ya Jericho ikiwa na usajili KE-KP 44333299 na risasi 15 alikamatwa.

Konstebo ndiyo ngazi ya chini zaidi katika kikosi cha polisi.

Dereva Enock Achami akiwa mwajiriwa wa serikali ya Kaunti ya Kakamega pia alitiwa mbaroni wakati wa operesheni hiyo.

Washukiwa hao wanne walidaiwa kumshambulia Chifu Inspekta Josphat Muia aliyekuwa ameandamana na maafisa wengine watatu katika doria ya barabara kuu ya Kisumu-Busia.

Shida inadaiwa kuzuka wakati walinzi hao wa gavana walionekana wakitoa bunduki kutoka kwa dirisha la gari lao la kiraia ili wapishwe nafasi ya kupita magari mengine.

Katika harakati hizo zao, waliomba nafasi ya kupita maafisa hao wa DCI ambao pia walikuwa ndani ya gari la kiraia.

“Maafisa wa DCI waliwakabili walinzi hao na baada ya kujitambulisha, wakawataka nao wajitambulishe ili wafahamiane lakini kukazuka purukushani iliyoingiliwa hata na wananchi,” ripoti ya Koome yasema.

Katika harakati hizo, Bw Muia aliingizwa kwa gari hilo la walinzi na akashambuluwa huku akitishwa kutupwa katika Mto Yala.

Lakini wenzake afisa huyo wa DCI waliita maafisa zaidi ambao waliwatia nguvuni walinzi hao wa gavana.

Sasa walinzi hao watajitetea mahakamani kwa kushambulia, kuchochea raia wapige maafisa wa polisi na kukaidi kutiwa nguvuni, ripoti hiyo yasema.

  • Tags

You can share this post!

Baadhi ya changamoto za wanafunzi katika mitaa ya mabanda

Namwamba awatuza wanahabari kwenye hafla ya kufana

T L