• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Obiri atawala Ras Al Khaimah Half, Koech aongoza wanaume 1-2-3

Obiri atawala Ras Al Khaimah Half, Koech aongoza wanaume 1-2-3

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Hellen Obiri na Benard Koech waliibuka washindi wa mbio za Ras Al Khaimah Half Marathon katika kisiwa cha Al Marjan nchini Milki za Kiarabu, Jumamosi.

Katika makala hayo ya 16 yaliyovutia wakimbiaji 5,500, mwanajeshi mkazi wa Amerika Obiri aliyekamilisha mbio hizo za kilomita 21 katika nafasi ya pili mwaka 2022, alitwaa taji la 2023 kwa saa 1:05:05.

Bingwa wa Afrika, Jumuiya ya Madola na dunia mita 5,000 Obiri alikuwa akishiriki mashindano yake ya kwanza barabarani mwaka huu. Alifuatwa kwa karibu na Waethiopia Gotytom Gebreslase (1:05:51) na Ftaw Bezabh (1:06:04) na Wakenya Brigid Kosgei (1:06:34) anayeshikilia rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42, na Evaline Chirchir (1:07:15) naye Agnes Mumbua akawa nambari saba (1:08:03).

Koech aliongoza Wakenya wenzake Daniel Mateiko na Richard Kimunyan walifagia nafasi tatu za kwanza katika kitengo cha wanaume kwa dakika 58:45, 58:49 na 59:37 mtawalia.

Wakimbiaji waliokamilisha katika nafasi tatu za kwanza walizawadiwa Sh1,713,501, Sh1,199,457 na Sh856,755 mtawalia. Muethiopia Gemechu Diriba (59:53) na Mmoroko Hicham Amghar (59:53) walifunga mduara wa tano-bora huku Wakenya wengine Weldon Langat (59:55), Ezra Tanui (saa 1:01:15), Vincent Kipchumba (1:06:13) na Geoffrey Kipsang (1:11:19) wakaridhika katika nafasi ya sita, tisa, 15 na 18 katika usanjari huo.

Wakenya wa mwisho kutawala Ras Al Khaimah Half Marathon kabla ya Obiri na Koech walikuwa Kibiwott Kandie na Fancy Chemutai mwaka 2020 na 2018 mtawalia. Ni mara ya kwanza Wakenya walifagia vitengo vyote viwili vya Ras Al Khaimah tangu Bedan Karoki na Chemutai mwaka 2018.

  • Tags

You can share this post!

Msimamizi wa kanisa achomoa kitambulisho cha askari jela...

Wanajeshi wa Ulinzi Starlets waahidi kupigana vilivyo...

T L