• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Obiri mawindoni Boston kusaka Sh19 milioni

Obiri mawindoni Boston kusaka Sh19 milioni

Na GEOFFREY ANENE

MKAZI wa Amerika, Hellen Obiri amethibitishwa kushiriki mbio za pili za Marathon Kuu Duniani (WMM) msimu huu Boston Marathon zitakazofanyika Aprili 17 nchini Amerika.

Mwanaolimpiki huyo, ambaye alihamia mjini Boulder mwaka jana na kupata kocha mpya Dathan Ritzenhein, alinyakua taji la United Airlines New York City Half Marathon hapo Machi 19.

Obiri, 33, atakuwa na mtihani mgumu katika jaribio lake la pili kwenye mbio za kilomita 42.

Waandalizi wa Boston Marathon wamesema kuwa Obiri atawania taji lililo na tuzo ya mshindi ya Sh19.8 milioni dhidi ya wakali Amane Beriso kutoka Ethiopia anayejivunia muda bora wa saa 2:14:58, mshindi wa Berlin Half Marathon 2022 Sheila Chepkirui (2:17:29), bingwa wa London Marathon 2021 Joyciline Jepkosgei (2:17:43) na malkia wa Amsterdam Marathon 2021 Angela Tanui (2:17:57) kutoka Kenya.

Pia, kuna Wakenya mshindi wa Ras Al Khaimah Half Marathon 2018 Fancy Chemutai (2:18:11), bingwa wa Boston Marathon 2017 Edna Kiplagat (2:19:50), mshindi wa Sanlam Cape Town Marathon 2019 Celestine Chepchirchir (2:20:10), bingwa wa Enschede Marathon Maurine Chepkemoi (2:20:18), nambari tatu Boston Marathon 2022 Mary Ngugi (2:20:22) na mshindi wa New York Marathon Sharon Lokedi (2:23:23).

Orodha ya washiriki pia ina Mwisraeli mwenye asili ya Kenya Lonah Salpeter aliyeshinda Tokyo Marathon kwa saa 2:17:45 mwaka 2020 na pamoja na bingwa wa dunia Gotytom Gebreslase kutoka Ethiopia (2:18:11), miongoni mwa wengine.

Mwanajeshi Obiri alikamilisha mashindano yake ya kwanza ya 42km katika nafasi ya sita wakati wa New York Marathon mwezi Novemba 2022.

Mfalme wa mbio za marathon Eliud Kipchoge anayeshikilia rekodi ya dunia ya wanaume ya saa 2:01:09 kutoka ushindi wake wa Berlin Marathon 2022, anaongoza orodha ya washiriki wanaume. Evans Chebet atatetea taji lake.

  • Tags

You can share this post!

Manchester City na Liverpool vitani kesho EPL

Malenga akariri mashairi yenye maudhui ya Ramadhani

T L