• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Malenga akariri mashairi yenye maudhui ya Ramadhani

Malenga akariri mashairi yenye maudhui ya Ramadhani

NA KALUME KAZUNGU

KUTANA na Hashim Said Mohamed, almaarufu DJ Fakhrudin,36.

Ni malenga aliyejitolea kuupamba msimu wa Ramadhani kisiwani Lamu kila unapowadia kupitia kutunga na kughani mashairi anayotumia kuwatumbuiza wazee, vijana kwa watoto.

Tungo zake za mashairi au tenzi ni nakshi tosha kwani huwa zimesheheni beti, mizani na mistari yenye vina tamutamu.

Mashairi yake huwa na jumbe, hotuba au maudhui sufufu yenye azma nzitonzito wakati huu wa kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Aghalabu waumini wengi wa dini ya kiislamu na mashabiki wa DJ Fakhrudin kisiwani Lamu huchukulia mashairi ya msanii huyo kuwa darasa tosha.

Utampata mshairi DJ Fakhrudin akiwa amejibanza, iwe ni barazani, kichochoroni, kishorobani mwa mji wa kale wa Lamu au hata ukumbini, huku akiwa amezingirwa na kandamnasi ya watu wa umri na haiba tofautitofauti, ikiwemo wazee waliokula chumvi nyingi, wale wa umri wa makamo, vijana na watoto au vitoto, hasa vile ambavyo vimeanza kusimama dede.

Wote hawa huwa wametega masikio yao kwa umakinifu mkuu na hata kujitia hamnazo kwa mengine yanayoendelea mjini, ilmradi watumbuizwe kwa mashairi yanayoghaniwa kwa sauti nyororo na yenye mnaso wa aina yake.

Katika mahojiano na Taifa Leo, malenga DJ Fakhrudin alikiri kuwa yeye hufanya hayo yote kwa kujitolea katika kuhakikisha waumini wa dini ya Kiislamu, na hata wale wasio Waislamu wanafanya mema; kusaidia wengine na hata kuwafanya walioko kwenye saumu kuwa ngangari zaidi wasilemewe na mfungo au kuasi kwa njia yoyote ile kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Maudhui kwenye ushairi wake kila wakati huwahimiza waja kutenda mema, kujitolea kusaidia maskini, wagonjwa, mayatima, wajane na wengineo wasiojiweza katika jamii ili kupokea thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Ikumbukwe kuwa Ramadhani ni mwezi wa tisa katika Kalenda ya Kiislamu.

Ni mwezi wa kufunga katika Uislamu kuadhimisha ufunuo wa kwanza wa Qur’an kutokana na mafundisho ya Mtume Muhammad (S.W.T).

DJ Fakhrudin anasisitiza kuwa yeye kila mwaka amekuwa akitumia siku zote, iwe ni 29 au 30 za Mwezi wa Ramadhani kutumbuiza waumini na wasio waumini kwenye mitaa mbalimbali ya kisiwa cha Lamu.

“Ramadhani, inayojumuisha kufunga ni mojawapo ya nguzo tano za Usislamu. Na hii ndiyo sababu mimi nimejitolea na kuifanya kawaida kama ibada hii hulka ya kutunga mashairi yangu na kuzurura vichochoroni, vibarazani na kwenye kumbi mbalimbali kuwatumbuiza wanaofunga na kuwahimiza kutenda mema, kuingia misikitini kuswali, kusoma Kurani na hata kuwasaidia wasiojiweza kwenye jamii zetu. Pia huhimiza waumini wajiepushe na tamaa za kidunia na badala yake wamwelekee Mwenyezi Mungu katika swala na toba zao,” akasema DJ Fahkrudin.

Miongoni mwa mashairi ambayo malenga huyo kayatunga na kuvuma nayo kisiwani, hasa yale ya maudhui ya Ramadhani ni; Karibu Mgeni Mwema-Mtukufu Ramadhani, Tufungeni Ramadhani-Mtukufu Mwezi Mwema, Waumini Ramadhanini-Someni Kurani na Ewe Mola Jalia-Ramadhani Enye Kheri.

Mshairi DJ Fakhrudin anashikilia kuwa hulka yake ya kuienzi na kuitii dini ndiyo iliyomsukuma kuanzisha harakati hizo.

Kulingana na yeye, mara nyingi msimu wa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani huwa kuna majaribu tele na waumini wengi hujipata wameteleza na kuanguka.

“Hivyo mimi hutumia mashairi yangu kuwakumbushakumbusha waja kuhusu umuhimu wa toba na kujisogeza karibu zaidi na Mola wetu kupitia ibada mbalimbali. Mashairi yangu husisitiza kuwa tukienda sawasawa basi tutavuna thawabu. Nashukuru kwamba harakati zangu zimeokoa wengi,” akasema DJ Fahkrudin.

Baadhi ya mashabiki kindakindaki wa msanii DJ Fakhrudin waliohojiwa na Taifa Leo hawakuficha furaha yao kuhusiana na juhudi za malenga huyo.

Kassim Shee,80, alisema mashairi ya DJ Fakhrudin huwafariji wengi ambao nyoyo huwa zimevunjika.

“Msanii DJ Fakhrudin ni kipenzi cha wengi hapa kisiwani. Mashairi yake yaliyokita mizizi hutupa matumaini hata wakati tunakumbana na uzito wa maisha au saumu. Pia ni hotuba tosha ya dini ya Kiislamu. Mimi binafsi sikosi kusikiliza mashairi yake karibu kila siku,” akasema Bw Shee.

Mohamed Haji anasema yeye binafsi tangu Ramadhani kuanza amejitahidi kusoma Kurani kwa wingi, hasa baada ya kupokea wosia kutoka kwa DJ Fakhrudin kupitia mojawapo ya mashairi yake.

“Huwezi kwenda kinyume na jambo fulani ikiwa kuna mja anayekukumbushakumbusha na hata kukuonya kama anavyotufanyia DJ Fakhrudin kupitia ughani wake wa mashairi,” akasema Bw Haji.

Kiongozi wa dini ya kiislamu Hamadi Mahamoud,85, alisema ni jambo jema kwa wasanii kama DJ Fakhrudin kujitolea na kutenga muda wao kuhudumia masuala yanayohusiana na dini.

Ustadh Mahmoud aliwashauri wasanii wengine, iwe ni malenga au waimbaji pia kuiga mfano wa DJ Fakhrudin kwa kutunga nyimbo za ibada na kumbukumbu kwa waumini hasa wakati wa Ramadhani na misimu mingine ya ibada.

Malenga DJ Fakhrudin alizaliwa kisiwa cha Kizingitini, eneobunge la Lamu Mashariki mnamo 1987.

Alisomea shule ya msingi ya Kizingitini kabla ya kujitosa kwenye usanii wa mashairi na muziki, hasa baada ya kukosa karo ya kuendeleza masomo yake kutokana na umaskini.

Ni mzawa wa saba katika familia ya watoto wanane.

Kipaji chake cha ushairi kilianza kuchipua mizizi alipokuwa darasa la nne, ambapo alikuwa akipewa fursa kuwatumbuiza wazazi na wageni wakati wa hafla za elimu shuleni kwao.

DJ Fakhrudin anatambulika sana kwa tungo zake, hasa kwenye majukwaa wakati wa kampeni mbalimbali za kisiasa Lamu na Pwani kwa jumla.

Ushairi wake umemwezesha kushiriki jukwaa moja na watu mashuhuri nchini, wakiwemo Rais Mstaafu hayati Mwai Kibaki, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Rais wa sasa Dkt William Samoei Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambao wote amewatumbuiza kupitia ughani wake wa mashairi.

DJ Fakhrudin pia anatambuliwa kwa kushiriki vipindi mbalimbali vya Kiswahili kwenye redio, ambapo hughani mashairi yake hewani.

Baadhi ya vituo vya redio ambavyo vimekuwa vikimpa fursa malenga DJ Fakhrudin kughani mashairi yake hewani ni idhaa ya Pwani FM, Redio Rahma, Bahari FM, Msenangu FM na Redio Lamu.

Ombi lake ni wahisani kujitokeza kumshika mkono ili kupalilia kipaji chake hata zaidi na kumwezesha kujipatia kipato kwani hadi sasa hana kazi ya kutegemea kumpatia mtaji wa kujikimu kimaisha isipokuwa ushairi.

  • Tags

You can share this post!

Obiri mawindoni Boston kusaka Sh19 milioni

Raila akaa ngumu, ampuuza Kindiki

T L