• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:50 AM
Ogallo na Muriu washindia Kenya shaba taekwondo za bara Afrika

Ogallo na Muriu washindia Kenya shaba taekwondo za bara Afrika

Na Geoffrey Anene

MKENYA Faith Ogallo aliridhika na medali ya shaba kwenye mashindano ya Afrika ya taekwondo yaliyoratibiwa kukamilika baadaye jana nchini Senegal.

Akishiriki kitengo chake cha uzani wa juu kabisa, mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Kibabii alianza mawindo ya medali vyema.

Ogallo alimlemea Niang Ami (Senegal) kwa alama 11-1 katika pigano la kwanza katika ukumbi wa Dakar.

Kisha alipoteza pembamba katika nusu-fainali dhidi ya Mmoroko Koutbi Sabah kwa jumla ya pointi 4-3 akipata shaba.Mshindi huyo wa medali ya fedha kwenye African Games 2019, ndiye mwakilishi wa Kenya katika Olimpiki za jijini Tokyo, Japan, zzitakazofanyika Julai 23 hadi Agosti 8.

Katika uzani wa unyoya, Mary Muriu alimlima Melouguo Meline kutoka Congo kwa pointi 30-8 katika pambano lake la kwanza, kabla yake kulimwa na Mmoroko Lasry Madam 15-3 kwenye nusu-fainali.

Wachezaji wengine kutoka Kenya waliokuwa ulingoni katika siku ya kwanza na ambao hawakufika nusu-fainali ni Emily Anyango, Newton Nambani Maliro, Edna Sichangi na Michael Ochieng’.

Wakenya wengine saba walipangiwa kuingia ulingoni baadaye jana pamoja na mkimbizi mmoja anayeishi Kenya na kudhaminiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR).

Wachezaji 297 kutoka mataifa 36 yakiwemo Misri, Tunisia, Morocco, Algeria, Senegal, Rwanda, Chad, Kenya, Niger na Botswana.

You can share this post!

Mbunge ashinikiza uchunguzi kuhusu dhuluma kwa wazee

Hazina ya NG-CDF kufadhili elimu ya wanafunzi vyuoni