• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:52 PM
Okutoyi aanza mazoezi nchini Australia baada ya vipimo kuondoa shaka ya Covid-19

Okutoyi aanza mazoezi nchini Australia baada ya vipimo kuondoa shaka ya Covid-19

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Angella Okutoyi amefanya mazoezi yake ya kwanza Jumanne mjini Melbourne, Australia baada ya kupatikana hajaambukizwa ugonjwa wa Covid-19.

Bingwa huyo wa Afrika kwa wachezaji chipukizi aliwasili Australia mnamo Jumatatu adhuhuri baada ya kuondoka jijini Nairobi mnamo Jumapili asubuhi.

Katika mahojiano Jumanne, Okutoyi ameeleza Taifa Leo, “Nilipimwa Covid-19 mara mbili baada ya kuwasili hapa. Uchunguzi wote umeonyesha niko sawa. Nilikuwa pia nimepokea chanjo zote zinazohitajika Nairobi. Kama ningepatikana na virusi hivyo bila shaka ningelazimika kujitenga ili kuzuia maambukizi. Nimefanya mazoezi ya kwanza hii leo.”

Okutoyi, ambaye anashikilia nafasi ya 60 kwenye viwango vya ubora vya chipukizi vya Shirikisho la Kimataifa la Tenisi (ITF), yuko katika orodha ya wachezaji 46 watakaowania taji la Australian Open la chipukizi mnamo Januari 22-29. Kabla ya hapo, Okutoyi,17, atawania ubingwa wa J1 Traralgon mnamo Januari 14-19.

Bingwa huyo wa Kenya Open mwaka 2018 alisema analenga kuandikisha matokeo mazuri nchini Australia na kukamilisha mwaka 2022 ndani ya wachezaji 30-bora duniani.

You can share this post!

Raila kuvumisha Azimio mjini Thika mnamo Jumamosi

Nigeria wazamisha Misri katika mechi ya Kundi D kwenye AFCON

T L