• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Olunga akwamilia juu ya jedwali la wafungaji Klabu Bingwa Asia, ana mabao sita baada ya kupachika mawili dhidi ya Esteghlal

Olunga akwamilia juu ya jedwali la wafungaji Klabu Bingwa Asia, ana mabao sita baada ya kupachika mawili dhidi ya Esteghlal

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Michael Olunga amedumisha uongozi wake juu ya jedwali la wafungaji wa mabao kwenye Klabu Bingwa Asia (Magharibi) baada ya kufungia Al Duhail mabao yote katika sare ya 2-2 dhidi ya Esteghlal nchini Saudi Arabia usiku wa kuamkia Jumapili.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alipata fursa ya kusawazisha 1-1 kupitia penalti iliyopatikana kabla tu ya kipindi cha kwanza kikatike ugani King Abdullah mjini Jeddah.

Vijana wa kocha Sabri Lamouchi walikuwa wamejipata bao moja chini baada ya wapinzani hao kutoka Iran kuchukua uongozi kupitia kwa raia wa Mali, Cheick Diabate ambaye pia alifuma wavuni penalti safi dakika ya 27.

Olunga maarufu kama Engineer, alipata bao la kuweka waajiri wake kutoka Qatar mbele 2-1 dakika ya 58 katika mechi hiyo ya Kundi C. Alipokea frikiki murwa kutoka nje ya kisanduku pembeni kulia na kumwaga kipa Mohammad Mazaheri kupitia kichwa.

Ngome ya Al Duhail ilitikiswa tena dakika tatu baadaye kupitia kwa Mehdi Ghayedi baada ya nahodha Voria Ghafouri kuchanja pasi safi ndani ya kisanduku.

Kufikia sasa, Mfungaji na Mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Japan mwaka 2020 Olunga amejaza wavuni mabao sita. Anafuatiwa na Omar Al Somah (Al Ahli Saudi) na Diabate ambao wamepachika manne kila mmoja.

Al Duhail wanaongoza jedwali kwa alama nane, moja mbele ya Esteghlal na wenyeji Al Ahli Saudi wanaotofautiana kwa ubora wa magoli. Al Shorta kutoka Iraq wako mkiani bila alama baada ya kupoteza michuano yao minne ya kwanza.

Vijana wa Lamouchi watakamilisha mechi zao za makundi dhidi ya Al Shorta (Aprili 27) na Ahli Saudi (Aprili 30).

Washindi wa makundi yote 10 wataingia moja kwa moja raundi ya 16-bora. Timu tatu zitakazokamilisha mechi za makundi za Ukanda wa Magharibi na pia Mashariki kwa alama nyingi pia zitaingia awamu ya muondoano.

You can share this post!

Hospitali ya Tigoni yatoa hewa ya oksijeni bure kwa wagonjwa

DINI: Tunapoishi na wenzetu tuachiane alama za moyoni,...