• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Omanyala, Chebet wafuzu kuwa polisi kutumikia umma

Omanyala, Chebet wafuzu kuwa polisi kutumikia umma

AYUMBA AYODI na AGNES MAKHANDIA

MABINGWA wa Jumuiya ya Madola Ferdinand Omanyala (mbio za mita 100) na Beatrice Chebet (5,000m) sasa ni maafisa wa polisi baada ya kufuzu katika mahafali kwenye Chuo cha Mafunzo ya Polisi cha Kiganjo, kaunti ya Nyeri, Jumanne.

Rais William Ruto aliongoza zoezi hilo ambapo makurutu 2,881 walifuzu.

Wanamichezo waliofuzu wanatoka katika fani ya riadha, voliboli, soka na taekwondo.

Wanaspoti zaidi wanatarajiwa kuhitimu katika mahafali yatakayofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi wa Utawala (APTC) na GSU mtaani Embakasi mnamo Alhamisi na Ijumaa mtawalia.

Bingwa wa Afrika na Jumuiya ya Madola 100m, Omanyala alifuzu pamoja na mshindi wa medali ya fedha ya Riadha za Dunia 5,000m Chebet aliyetawala Jumuiya ya Madola.

Wanariadha wengine waliofuzu ni mshindi wa nishani ya fedha ya Jumuiya ya Madola 10,000m Daniel Simiu na shaba ya 1,500m ya Riadha za Dunia za Ukumbini Abel Kipsang.

Pia, kuna bingwa wa taifa wa kurusha mkuki Martha Musai pamoja na Agnes Ngumbi (400m kuruka viunzi), Nancy Kanini (Hammer), Caroline Chepkorir (3,000m kuruka viunzi na maji), Elijah Kibet (5,000m), Robert Kiprop (5,000m) na Nobert Kolombos (800m).

Mchezaji wa timu ya taifa ya voliboli ya Malkia Strikers, Carolyne Sirengo alifuzu baada ya miezi tisa ya mafunzo ya polisi. Yeye ni miongoni mwa wachezaji 14 wa klabu ya Idara ya Upelelezi (DCI) waliohitimu. Wengine ni Marion Indeche, Jemimah ‘Magereza’ Siangu, Jane Mumbai, Peris Kanus, Mercy Iminza, Christabel Siyuyu, Sarah Nakhulicha, Abigael Nafula, Joan Baraza, Joy Wangaya, Carolyne Cheruto, Peninah Nafula na Benedine Chemwetich.

Kocha wa timu hiyo ya voliboli ya DCI, Daniel Bor alishukuru Idara ya Polisi kwa kuwapa nafasi hizo 14 za kazi.

“Hii imeturahisishia kazi na sasa tutamakinikia tu kucheza. Visa vya wachezaji kukosa nauli kufika mazoezini sasa havitakuwa kwa sababu wamepata kazi. Natumai wachezaji sasa “watarudisha mkono” kwa kutuletea matokeo mazuri,” alisema Bor. Meneja wa timu hiyo Neddy Nelimo alisifu hatua hiyo akisema itainua mchezo wa voliboli.

DCI, Kenya Pipeline, KCB na Kenya Prisons zitawania ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kuingia katika awamu ya nne-bora itakayosakatwa Januari 20-22 ukumbini Kasarani ambapo timu mbili-bora zitajikatia tiketi kushiriki mashindano ya Afrika.

Baadhi ya watakaofuzu APTC ni wanaraga wa kimataifa Jeffrey Oluoch, Levi Amunga na Collins Shikoli, na wakimbiaji Hyvin Chepkemoi, Newton Kipng’etich na Samuel Naibei.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Sabuni ya Kenya Kwanza

Gavana wa zamani aagizwa ampe mwanamke Sh236,000 kila mwezi...

T L