• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Otieno aelekea Kampala kutafuta tiketi ya Olimpiki ya mbio fupi baada kufeli Zambia

Otieno aelekea Kampala kutafuta tiketi ya Olimpiki ya mbio fupi baada kufeli Zambia

Na AYUMBA AYODI

MTIMKAJI wa mbio fupi Mark Otieno atakuwa mawindoni mjini Kampala kwa mashindano ya kitaifa ya Uganda hapo Jumamosi kutafuta tiketi ya Olimpiki.

Otieno, ambaye yuko katika timu ya Kenya ya Riadha za Dunia za kupokezana vijiti ya mbio za mita 4×200, atashiriki mbio za mita 100 na mita 200 ugani Namboole.

Mwenzake kwenye timu hiyo ya kupokezana vijiti Mike Mokamba, ambaye pia alifaa kuenda Uganda kutafuta tiketi ya Olimpiki ya mbio za mita 200, hakufaulu baada ya kukosa kupata pasipoti ya kusafiria kwa muda ufaao.

Otieno alikaribia kufuzu kushiriki Olimpiki katika mbio za mita 100 aliposhinda taji la mashindano ya All Comers wiki chache zilizopita uwanjani National Heroes mjini Lusaka, Zambia.

Otieno alipata kuimarisha rekodi yake ya kitaifa kwa sekunde 0.3 akitwaa taji kwa sekunde 10.11. Alikosa muda wa kuingia Olimpiki wa mbio za mita 100 kwa sekunde 0.06. Katika nusu-fainali, Otieno alikuwa ameandikisha sekunde 10.19 akishinda mchujo wa kitengo chake.

Kazi yake katika fainali ilishuhudia akifuta muda wake bora wa awali wa sekunde 10.14 alioweka akishinda ubingwa wa Kenya mwaka 2017.

Otieno alitimka mbio za mita 200 kwa muda wake mzuri msimu huu wa sekunde 20.46 akitawala kitengo hicho mjini Lusaka.

Muda ya kuingia Olimpiki wa mbio za mita 100 na mita 200 ni sekunde 10.05 na sekunde 20.24, mtawalia.

“Natumai nitafaulu mjini Kampala. Nitafurahi nikipata muda wa kuingia Olimpiki ninapojiandaa kuelekea mjini Silesia nchini Poland kwa Riadha za Dunia za kupokezana vijiti. Sina presha,” alisema Otieno kabla ya kuyoyomea Uganda.

Otieno bado anashikilia rekodi ya kitaifa ya mbio za mita 100 baada ya Shirikisho la Riadha Kenya (AK) kukataa kurasimisha muda wa Ferdinand Omanyala aliyekamilisha umbali huo kwa sekunde 10.01 akishinda nusu-fainali yake kwenye mashindano ya Betking MoC Grand Prix ugani Yabatech Complex mjini Lagos, Nigeria mnamo Machi 30.

Wakati huo huo, timu ya Kenya itapokea chanjo ya mwisho ya kuzuia ugonjwa wa Covid-19 hapo Aprili 24 kabla ya kujua nani ataabiri ndege ya kuelekea Silesia kwa Riadha za Dunia za kupokezana vijiti.

Mkurugenzi wa mashindano wa AK, Paul Mutwii alifichua kuwa wenyeji Poland watahitaji vyeti vya Covid-19 mara tu timu itawasili.

Timu ya wakimbiaji 32 na maafisa 16 inatarajiwa kuondoka nchini mnamo Aprili 28 ikiongozwa na rais wa AK, Jack Tuwei.

“Shughuli ya kupimwa itakuwa muhimu sana na tunajaribu sana kuona timu hii haitangamani na watu kutoka nje,” alisema Mutwii ambaye alikuwa mwingi wa matumaini kuwa watimkaji wa Kenya watafanya vyema baada ya kuwa kambini tangu Machi 1.

Kenya iliambulia medali moja pekee katika makala yaliyopita mjini Yokohama, Japan ambayo ni shaba ya mbio za mita 4×400 za mseto.

Mshindi wa nishani ya shaba ya mbio za mita 800 Ferguson Rotich na bingwa wa mbio za mita 800 wa michezo ya Jumuiya ya Madola Wycliffe Kinyamal pamoja na wakimbiaji wa mbio za mita 400 Zablon Ekwam na Mary Moraa wameungana na wenzao kambini.

Rotich na Kinyamal wako katika mbio za 2x2x400 ambazo pia ziko na Naomy Jerop na Emily Cherotich naye Moraa atashirikiana katika mbio za 4×400 za wanawake na 4×400 za mseto.

You can share this post!

Nitampigia Rais simu baada ya kujuzwa hali yake na mkewe...

Rufina (Mama Silas) aelezea safari yake ya uigizaji