• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Patson Daka: Fowadi matata wa Zambia anayenyima miamba wa soka barani Ulaya usingizi

Patson Daka: Fowadi matata wa Zambia anayenyima miamba wa soka barani Ulaya usingizi

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United, Liverpool na Arsenal wanaongoza orodha ya vikosi vinavyowania maarifa ya mwanasoka matata raia wa Zambia, Patson Daka, ambaye kwa sasa anachezea Red Bull Salzburg ya Austria.

Daka amekuwa kivutio cha makocha wa klabu nyingi za bara Ulaya baada ya kujivunia msimu wa kuridhisha kambini mwa waajiri wake ambapo amefuma wavuni jumla ya mabao 27 kutokana na mechi 31 zilizopita katika mashindano yote.

Kufikia sasa, sogora huyo ndiye anayeongoza orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu ya Austria kwa mabao 20 kutokana na mechi 18.

Daka, 22, alifungia Salzburg mabao mawili kwenye michuano miwili ya kirafiki dhidi ya Liverpool mnamo Agosti 2020. Alipachika wavuni magoli mawili katika ushindi wa 5-2 uliosajiliwa na waajiri wake dhidi ya Maccabi Tel Aviv ya Israel mnamo Septemba 2020 na kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Japo Salzburg wamesisitiza kwamba hawana nia ya kumtia Daka mnadani hivi karibuni, huenda wakashawishika kumuuza na Manchester City tayari wamesema wako radhi kuweka mezani kima cha Sh2.4 bilioni kwa minajili ya huduma za sogora huyo. Bayern Munich, PSG na Barcelona ni vikosi vingine vinavyomhemea Daka.

Kocha wa timu ya taifa ya Zambia, Milutin Sredejovic, amesema kwamba ukubwa wa uwezo wa Daka ambaye anapata msukumo mkubwa kutoka kwa jagina wa soka wa Cameroon, Samuel Eto’o, unaweza kulinganishwa na upekee wa makali ya Pierre-Emerick Aubameyang (Arsenal), Mohamed Salah (Liverpool) na Sadio Mane (Liverpool).

Kinachowapa Man-United msukumo wa kumsajili Daka ni ulazima wa kujaza pengo la fowadi Edinson Cavani ambaye anatarajiwa kurejea Argentina kuvalia jezi za Boca Juniors mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Salzburg inajivunia kupokeza malezi ya soka wanasoka Dominik Szoboszlai, Takumi Minamino na Erling Haaland waliyoyomea RB Leipzig, Liverpool na Borussia Dortmund mtawalia mwanzoni mwa Januari 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Waititu asema yuko ndani ya Kieleweke na Handisheki

SHINA LA UHAI: Corona: Chanjo ya AstraZeneca ni salama?