• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Poland na Uingereza nguvu sawa katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia

Poland na Uingereza nguvu sawa katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia

Na MASHIRIKA

POLAND walisawazisha katika dakika za mwisho za mchezo na kuwanyima wageni wao Uingereza alama tatu muhimu na ushindi wa sita mfululizo kwenye kampeni za Kundi I kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Uingereza waliweka uongozini na nahodha Harry Kane katika dakika ya 72 baada ya kumwacha hoi kipa Wojciech Szczesny.

Jaribio la Poland kurejea mchezoni kupitia fowadi matata Robert Lewandowski lilikosa kuzaa matunda baada ya mabeki wa Uingereza kumbana ipasavyo.

Hata hivyo, masihara ya difenda Luke Shaw sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa yalimpa Damian Szymanski fursa ya kusawazisha mambo baada ya kumzidi ujanja kipa Jordan Pickford.

Bao hilo lilikuwa pigo kubwa kwa Uingereza walioshuhudia idadi kubwa ya wachezaji wao wakiondoka uwanjani wakiinamisha vichwa kwa aibu. Ilikuwa matarajio ya mashabiki kwamba Uingereza wangeondoka jijini Warsaw na alama tatu muhimu hasa ikizingatiwa jinsi walivyotamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira.

Licha ya sare hiyo, Uingereza wangali kileleni mwa Kundi I kwa alama 16, nne zaidi kuliko nambari mbili Albania. Zimesalia mechi nne pekee kwa kampeni za kuwania tiketi za kuelekea Qatar mnamo 2022 kwa fainali za Kombe la Dunia kutamatika.

Poland wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 11, moja kuliko Hungary wanaowazidi Andorra kwa pointi saba. San Marino wanavuta mkia bila pointi yoyote.

Bao la Kane lilikuwa lake la 41 ndani ya jezi ya Uingereza na kwa sasa ndiye anashikilia nafasi ya tano kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote kambini mwa kikosi hicho. Goli lake dhidi ya Poland lilimwezesha kuweka rekodi ya kufunga katika mechi 15 mfululizo za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia na Euro.

MATOKEO YA SEPTEMBA 8, 2021:

Iceland 0-4 Ujerumani

Kosovo 0-2 Uhispania

Italia 5-0 Lithuania

N.Ireland 0-0 Uswisi

Belarus 0-1 Ubelgiji

Wales 0-0 Estonia

Poland 1-1 Uingereza

Armenia 1-1 Liechtenstein

Macedonia Kaskazini 0-0 Romania

Ugiriki 2-1 Uswidi

Albania 5-0 San Marino

Hungary 2-1 Andorra

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Vihiga Queens waibuka malkia wa Cecafa, wapokea Sh3m na...

Jinsi ya kuondoa harufu mbaya kwenye jokofu