• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
Vihiga Queens waibuka malkia wa Cecafa, wapokea Sh3m na kuingia Klabu Bingwa Afrika

Vihiga Queens waibuka malkia wa Cecafa, wapokea Sh3m na kuingia Klabu Bingwa Afrika

Na GEOFFREY ANENE

VIHIGA Queens wamejikatia tiketi ya kushiriki makala ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kuduwaza wanabenki wa CBE 2-1 kwenye fainali ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ugani Kasarani, Alhamisi.

Katika mechi hiyo iliyohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Fatma Samoura, mshambuliaji matata Jentrix Shikangwa alipachika mabao yote mawili.

Alifungua ukurasa wa magoli dakika ya 26 baada ya kipa Tarikua Bargena Balcha kutema mpira kabla ya kufunga la ushindi kupitia penalti dakika ya mwisho iliyopatikana wakati Violet Wanyonyi aliangushwa kisandukuni.

Vipusa wa kocha Charles Okere na Boniface Nyamunyamu, ambao walipigwa 4-2 na Waethiopia katika mechi za Kundi B, walitawala mchuano huo ikiwemo Tereza Engesha na Shikangwa kugonga mpira kwenye mwamba. Waethiopia walipata bao lao baada ya Vivian Makokha kujifunga dakika ya 53.

Shikangwa aliibuka mchezaji bora wa mashindano hayo yaliyovutia klabu nane kutoka mataifa ya Kenya, Ethiopia, Uganda, Tanzania, Burundi na Djibouti pamoja na Zanzibar.

Vihiga walizawadiwa Sh3,297,900. CBE waliridhika na Sh2,198,600 nao Lady Doves kutoka Uganda waliolima Simba Queens ya Tanzania 2-1 katika mechi ya kutafuta nambari tatu, wakatia mfukoni Sh1,099,300.

Vihiga wameungana na wenyeji Wadi Degla SC (Misri) pamoja na AS FAR kutoka Morocco (washindi wa Muungano wa Kaskazini mwa Afrika), AS Mande kutoka Mali (washindi shindano la kwanza la Muungano wa Magharibi mwa Afrika), Hasaacas Ladies kutoka Ghana (washindi shindano la pili la Muungano wa Magharibi mwa Afrika) na Rivers Angels (nambari mbili katika shindano la pili la Muungano wa Magharibi mwa Afrika).

Washindi kutoka Muungano wa Afrika ya Kati kati ya Malabo Kings (Equatorial Guinea) na FCF Amani (DR Congo) pamoja na Baraza la Mashirikisho ya Soka ya Kusini mwa Afrika (Cosafa) Mamelodi Sundowns Ladies pia walifuzu Klabu Bingwa Afrika ya wanawake itakayofanyika Novemba na Desemba nchini Misri.

“Hatukuwa wazuri katika ulinzi katika mechi ya kwanza, lakini tuliiimarisha na pia Mungu atatubariki na magoli,” alisema Nyamunyamu baada ya mechi akiongeza kuwa sasa watazamia mazoezi ya Klabu Bingwa ambayo alikiri haitakuwa rahisi.

Shikangwa alisema kuwa Vihiga iliingia mechi hiyo ikifahamu kuwa lazima waishinde ili kufuzu. “Hata baada ya CBE kusawazisha, tulikuwa na imani tunaweza kuibuka na ushindi,” alisema na kuongeza kuwa hakuwa na presha kupiga penalti. Aliahidi kuwa Vihiga itajitahidi kupata matokeo mazuri nchini Misri.

Raia wa Ethiopia Loza Geinoire aliibuka mfungaji bora kwa kuchana nyavu mara 13.

You can share this post!

AKILIMALI: Mkenya ajizolea tuzo ya Sh165 milioni atumie...

Poland na Uingereza nguvu sawa katika mechi ya kufuzu kwa...