• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Raila, mashabiki walaani mauaji ya kipenzi Juma

Raila, mashabiki walaani mauaji ya kipenzi Juma

JOHN ASHIHUNDU na SHABAN MAKOKHA

MASHABIKI na wapenzi wa soka nchini waliendelea kulaani vikali mauaji ya shabiki sugu Isaac Juma, 55, nyumbani kwake Mumias mnamo Jumatano usiku.

Aidha, maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wamemtia mbaroni mmoja wa washukiwa wa mauaji hayo ya kinyama.

Maafisa walimnasa Milton Namatsi, 27, nyumbani kwake baada ya uchunguzi wa awali kumhusisha na mauaji ya shabiki huyo mkubwa wa klabu ya AFC Leopards na timu ya taifa Harambee Stars.

Kinara wa ODM Raila Odinga, ambaye pia ni shabiki sugu wa soka na mlezi wa klabu ya Gor Mahia, anataka maafisa wa usalama kufanya hima kuhakikisha wote waliohusika wamenaswa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

“Alileta uchangamfu uwanjani na kufanya mechi za AFC Leopards kuwa za kusisimua,” alitanguliza Odinga katika taarifa yake Alhamisi jioni.

“Maafisa wafanye haraka kukamata wahusika wa ukatili huu. Lazima tuonyeshe wazi kwamba unyama huu hauna nafasi katika jamii yetu,” aliongeza kigogo huyo wa siasa na kutoa rambirambi zake kwa familia, klabu ya Leopards na fani nzima ya soka nchini.

Mlezi wa Leopards, Musalia Mudavadi, pamoja Naibu Rais William Ruto pia walituma risala zao.

Juma na familia yake walikuwa waenda kulala muda mfupi tu nyumbani kwake katika kijiji cha Bukaya, Mumias, wauaji walipowavamia.

Awali usiku huo, watoto wakila nje walieleza kuona vivuli vya watu kwenye ua la nyumba.

Wakaingia kuwafahamisha wazazi wao, ambao hawakuchukulia maneno yao kwa uzito.

Muda mfupi baada ya kwenda kulala walisikia mvurugano katika zizi la kondoo.

Juma, nduguye na mvulana wake wa umri wa miaka 17 walipoenda kutazama kilichojiri, walikumbana na genge lililowashambulia kwa mapanga na kumuua shabiki huyo.

Mvulana huyo na ndugu ya marehemu waliponyoka kifo padogo baada ya kutorokea upande wa shamba.

Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Mumias Magharibi, Stephen Muoni, alisema Juma alifariki papo hapo.

“Lengo la genge hilo halikuwa kuiba mifugo bali kuua,” aliongeza Muoni.

Mwili wa marehemu ulipatikana nje ya nyumba yake ukiwa umevuja damu, kabla maafisa kuupeleka mochari ya hospitali ya St Mary’s.

Makachero wanahisi kifo cha Juma kinahusiana na mzozo wa ardhi ambao umekumba familia yake.

Shabiki huyo wa kandanda alikuwa mwuzaji gazeti mjini Nakuru kabla kustaafu nyumbani kwake Mumias.

Alishabikia Stars na timu ya AFC Leopards kwa upekee.

Chama cha Mashabiki wa Soka Nchini (Kefofa) kupitia kwa Afisa Mkuu Shem Okottah kilitaja kifo cha Juma kama pigo kubwa kwa muungano wao, huku akisema watamkumbuka jinsi alivyoshabikia Stars.

Okottah alisema: “Alikuwa shabiki nambari moja. Alisononeka kila wakati timu iliposhindwa. Tunasema makiwa kwa familia.”

Msemaji wa Kamati ya Muda ya Soka Kenya, Ali Amour, alihoji kwamba Juma alikuwa mzalendo na shabiki sugu aliyechangamsha watu ugani.

“Kama viongozi wa soka, tulipokea habari za kifo chake kwa mshtuko mkubwa,” alisema Amour.

Kwenye jumbe zao, Musalia na Ruto pamoja na Seneta wa Siaya, James Orengo, walisema kuwa marehemu alijulikana kwa kuwa shabiki mkubwa na mpenzi sugu wa kandanda, aliyepatikana uwanjani kila wakati kushangilia timu yake.

Nao Twaha Mbarak na Milton Nyakundi, ambao wametangaza kuwania urais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF), pia walituma pole zao. Wameitaka DCI kuhakikisha wahusika wote wanakabiliwa vikali.

“Marehemu ni miongoni mwa mashabiki wachache walioufanya mchezo kuvutia zaidi. Rekodi yake katika uimarishaji wa kandanda nchini itakumbukwa milele,” alisema Twaha.

“Tungependa Serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi Nchini (DIC) itilie mkazi uchunguzi kuhusu kifo cha Juma na kuhakikisha wahusika wamekabiliwa vikali kisheria,” alisema Nyakundi.

Mnamo Novemba 2011, alikuwa miongoni mwa Wakenya waliotwaa tuzo kutokana na mchango wake katika kuimarisha kandanda nchini. Kwa kushinda tuzo hiyo ya shabiki bora, Juma aliondoka na Sh100,000.

Juma anayesemakama kuaua kutokana na mzozo wa ardhi amewaacha wajane Christina na Faridah pamoja na watoto 10.

You can share this post!

Jepkorir, Mateiko kuwa kivutio mbio za nyika za Discovery...

DOMO: Malipo hapa hapa duniani!

T L